Vyama vitakavyoshiriki uchaguzi marudio Zanzibar

Vyama vitakavyoshiriki uchaguzi marudio Zanzibar

    VYAMA vitano vya siasa vitashiriki katika uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, utakaofanyika Machi 20 mwaka huu, uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ADC, CCK, TLP na SAU.
Hatua hiyo inatokana na vyama vitatu vya siasa Zanzibar vya CCK, SAU na TLP, kutangaza kuwa wagombea wake, watashiriki katika uchaguzi huo wa Machi 20. Taarifa ya viongozi wa vyama vya CCK, SAU na TLP, iliyosomwa kwa pamoja katika Ukumbi wa Culture eneo la Mji Mkongwe mjini hapa jana, ilisema wagombea wa vyama hivyo vitatu, watashiriki uchaguzi huo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ulifutwa baada ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali, zilizoonesha wazi kwamba hauwezi tena kuwa huru na haki. Wagombea wa vyama hivyo vya siasa, waliotangaza kushiriki katika uchaguzi huo ni Ali Khatib kutoka CCK, Issa Mohamed Zonga kutoka SAU na Hafidh Hassan Simai kutoka TLP.
Mgombea wa CCK, Ali Khatib Ali alisema kwamba tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi huo na kuwataka wanachama na wafuasi wake na wananchi, kuitumia fursa hiyo ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaoongoza nchi. “Tangazo la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) limetutaka kurudia uchaguzi kwa sababu ule wa awali umefutwa kwa hivyo hatuna sababu ya kususia uchaguzi huo na tunachofanya kwa sasa ni kuwataka wanachama wetu na wafuasi kujitayarisha kwa uchaguzi wa marudio,” alisema Ali.
Jumapili iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema chama hicho kipo tayari kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 kwa lengo la kuhakikisha kinashika dola. Akihutubia mamia ya wanachama wao katika viwanja vya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui wakati wa kuzindua maadhimisho ya miaka 39 ya CCM, Dk Shein alisema maamuzi ya kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu, yamefanywa na ZEC ambayo ndiyo chombo halali kwa mujibu wa Katiba cha kushughulikia masuala yote ya uchaguzi nchini.
Aliwataka wanachama na wafuasi wao kujipanga vizuri na kushiriki uchaguzi huo kikamilifu, kwani kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni kushinda chaguzi zote zinazofanyika nchini ili kushika dola na kuwatumikia wananchi. “Hayo ndiyo maamuzi ya chama chetu tuliyokubaliana kushiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio baada ya kufutwa kwa ule wa Oktoba 25 mwaka jana kwa hivyo wanachama na wafuasi jitayarisheni kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kushika dola,” alisema Dk Shein.
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam limevisihi vyama vya siasa vya Zanzibar kikiwemo Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kimetangaza kususia uchaguzi wa marudio, kushiriki uchaguzi huo kwa maslahi ya Taifa. Aidha, limeitaka ZEC kuhakikisha inasimamia uchaguzi huo kwa haki, uadilifu na umakini mkubwa huku wakimuogopa Mungu na kutambua kuwa kama hawatatenda haki, wataulizwa katika siku za mwisho.
Hayo yalielezwa na Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana. Alieleza kuwa Baraza hilo, haliwezi kukaa kimya kana kwamba suala la Zanzibar haliwahusu Watanzania Bara, bali linawahusu Watanzania wote kwa kuwa ni ndugu wa damu. “Sisi Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam tunaunga mkono hatua ya ZEC kufanya uchaguzi wa marudio...vile vile tunakiomba chama cha CUF ambacho kimetangaza kususia uchaguzi huo na vyama vingine vyote, viache kususia bali vijipange kwa ajili ya kushiriki.
“Lakini pia tunawaomba ZEC kulisimamia zoezi hilo kwa haki na umakini mkubwa kwa maslahi ya taifa... pia wamuogope Mungu wakumbuke hii dunia tunapita, wasipotenda haki wataulizwa na Mwenyezi Mungu kwanini walisimamia batili,” alisema Shehe Salum. Aidha, alisema barua aliyoipokea kutoka kwa Amir wa Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmad ambaye yuko gerezani, imeeleza kuwa anaunga mkono suala la kufanya uchaguzi wa marudio kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kumaliza mgogoro huo, na kuwa hakuna njia mbadala.
Alisema katika barua hiyo, Shehe Farid aligusia mambo matatu ambapo hata hivyo mambo mengine mawili ambayo yameandikwa katika barua hiyo, hakuyataja yalizungumzia nini. Aliwataka Wazanzibari kuhakikisha wanadumisha amani na utulivu walionao na kulinda umoja na mshikamano, kwani amani itakapovurugika, haitaishia Zanzibar pekee, bali itagusa hadi Bara hivyo wanatakiwa kuwa watulivu.
Aidha, Bakwata imepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli kutokana na hatua mbalimbali inazozichukua, zenye lengo la kuimarisha nidhamu, hasa kwa watumishi wa umma na serikali. Shehe Salum alisema hatua hizo, zimeanza kuleta tija kubwa kwa taifa kwani hata pato la serikali limekuwa likiongezeka mwezi hadi mwezi.
Aidha, baraza hilo limeiomba serikali kuendelea kutatua changamoto mbalimbali hasa zilizoko ndani ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwemo kulipa umuhimu unaostahili Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kwani suala la foleni linachangia kuzorotesha uchumi wa Taifa kutokana na kuwa wafanyakazi wengi wanategemea usafiri wa daladala.
“Aidha, tunapongeza dhamira yake ya kubana matumizi ya serikali na badala yake kuelekeza fedha kwenye huduma za jamii na tayari tumeshaanza kunufaika na huduma hizo,” alisema. Alisema huduma hizo ni pamoja na elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, kwani linalopaswa kupongezwa kwa kuwa ada za shule na gharama za kuandikisha watoto zilikuwa ni mzigo kwa wananchi wengi.
“Ni muhimu Serikali kuwasaidia wawekezaji wa ndani kama hawa Simon Group, wamefanya kazi nzuri na kama kuna masharti magumu wamewekewa serikali ione namna ya kuwasaidia kwa kuwa wananchi wanahitaji usafiri huo wa mabasi ya mwendo kasi ili waondokane na adha ya foleni, walete ufanisi katika kazi zao.
Ndivyo wanavyofanya duniani kote wawekezaji wa ndani wanasaidiwa,” alisema Shehe wa Mkoa. Imeandikwa na Katuma Masamba, Dar na Khatib Suleiman, Zanzibar

 

 

Miaka 52 ya Mapinduzi

Miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar

 WAZANZIBARI  wamesherehekea miaka 52 ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964, ambayo yaling’oa utawala wa Sultani kutoka Oman na kuwezesha wazalendo wengi kushika hatamu ya kuongoza nchi.

Katika kilele cha sherehe hizi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein atahutubia taifa katika uwanja wa Amaan.

Matukio mengine makubwa yaliyofanyika katika uwanja huu ni Rais Shein kukagua gwaride la heshima la vikosi ya ulinzi na usalama, vikiongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Amepokea maandamano ya wananchi wa mikoa mitano ya Unguja.

Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu na Viongozi wastaafu, Mzee Mwinyi, Benjamin Mkapa Aman Karume na Wengine Wengi wa Kitaifa, wamewasili uwanja wa Amani katika sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Z'bar.

Vilevile Mkuu wa Majeshi Mwamnyange amehudhulia. Viongozi wengi wa Kitaifa wamehudhulia.

 

 Rais Magufuli atengua uteuzi wa Dk. Hoseah

Rais Magufuli atengua uteuzi wa Dk. Hoseah 

 

RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk Edward Hoseah. Aidha, ameamuru kusimamishwa kazi kwa watumishi waandamizi wanne wa taasisi hiyo kwa kukiuka maagizo yake.
Rais ametengua uteuzi huo wa Dk Hoseah, kutokana na kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa, hususan kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam jana kwa niaba ya Rais, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alisema kutokana na kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.
Balozi Sefue alibainisha kuwa Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa Takukuru chini ya Dk Hoseah, hauwezi kuendana na kasi anayoitaka.
“Eneo mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya serikali ni bandarini na katika Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, hivyo Mheshimiwa Rais amesikitishwa na kitendo cha taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika eneo hilo kwa muda mrefu, lakini kasi ya Takukuru kuchukua hatua haiendani na kasi anayoitaka,” alisisitiza Balozi Sefue.
Dk Hoseah alichaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru mwaka 2006, na hivyo amedumu katika wadhifa huo kwa takribani miaka tisa sasa. Alitanguliwa na Meja Jenerali mstaafu, Anatory Kamazima ambaye aliiongoza Takukuru kuanzia mwaka 1990 hadi 2006.
Wakurugenzi wengine waliowahi kuiongoza Takukuru ambayo awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) ni Geofrey Sawaya (1973 – 1974), S. Rutayangirwa (1974 – 1975) na Zakaria Maftah (1975 – 1990).
Kwa mujibu wa sheria, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru huteuliwa na Rais, na anasaidiwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu, wadhifa alionao Mlowola ambaye kabla ya uteuzi huo uliofanywa Oktoba 23, mwaka huu, alikuwa Mkurugenzi wa Intelijensia ya Makosa ya Jinai katika Jeshi la Polisi nchini.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Takukuru waliosafiri nje ya nchi, licha ya Rais kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.
Watumishi hao ni Mkurugenzi Elimu kwa Umma, Mary Mosha, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Ekwabi Mujungu, Mkurugenzi wa Uhusiano, Doreen Kapwani na Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi Mkuu, Rukia Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Kutokana na hatua hiyo ya Rais Magufuli, Balozi Sefue amewataka watumishi wengine wa umma, kutii agizo la Rais na kuonya kuwa atakayekiuka atachukuliwa hatua kali. Katika moja ya hatua za kubana matumizi ya serikali, Rais Magufuli alitangaza kufuta safari zote za nje kwa watumishi wa umma, isipokuwa kwa vibali maalumu.

Rais Magufuli atangaza baraza la Mawaziri

Rais Magufuli Atangaza baraza la Mawaziri

Vioongozi wakuu wa Serikali

Mawaziri Hao ni


Wizara ya Mambo ya Nje na EAC/ Kimataifa
Waziri- Augustino Mahiga, Naibu Waziri - Dk. Suzan Kolimba

Wazara wa Utamaduni, Sanaa na michezo
Waziri-Nape Nnauye

Wizara ya Nishati na Madini
Waziri -Sospeter Muhongo na Naibu Waziri-Medard Kalemani

Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu
Waziri -Jenista Mhagama

Wizara ya ofisi ya Rais, Utumishi na utawala
mawaziri wawili - Simbachawene na Kairuki

Ofisi ya Makamu wa Rais/Muungano na Mazingira
Waziri - January Makamba Naibu waziri Luhaga Mpina.

Wizara ya Mambo ya Ndani
Waziri ni Charles Kitwanga

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi
Waziri wake ni Wiliam Lukuvi Naibu Angelina Mabula.

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Waziri - Husein Mwinyi

Wizara ya Katiba na Sheria
Waziri - Harrison Mwakyembe

Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
Waziri - January Makamba

Wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi
Waziri- Mwigulu Nchemba Naibu Waziri- William Tate Ole Nashon

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Waziri - Charles Mwijage

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Waziri - Ummy Mwalimu - Naibu - Dk Hamis kigwangalla

Wizara ya Sayansi, Teknolojia, Elimu na Ufundi
Waziri - bado hajapatikana - Naibu Waziri -Stela manyanya

Wizara ya Maliasili na Utalii
Waziri - bado hajapatikana na Naibu Waziri - Injinia Ramo Makani

Waziri wa Fedha na Mipango
Waziri - bado hajapatikana, Naibu Waziri - Dk. Ashantu Kijachi

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Waziri - bado hajapatikana, Naibu Waziri -Edwin NgonyaniSerikali yachunguza ufisadi wa dola mil 6

Serikali yachunguza ufisadi wa dola mil 6

SERIKALI inachunguza ufisadi wa Dola za Marekani milioni sita, ambazo Benki ya Stanbic Tanzania pamoja na Kampuni ya Egma ya nchini, iliongeza katika malipo ya ada ya mkopo, ambao Serikali iliomba kwa Benki ya Standard ya Uingereza mwaka 2013.
Imesema inafanya uchunguzi wa ndani ili kubaini fedha hizo za kigeni zilizoingizwa kwenye akaunti ya Egma, zimekwenda wapi na kama zilitumika kuhonga, zimemhonga nani. Akizungumza na waandishi wa habari jana Ikulu Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hatua hiyo imekuja baada ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO) kushinda kesi katika Mahakama ya Southwark Crown ya Uingereza dhidi ya Stanbic Tanzania inayomilikiwa na Standard Group.
“Sasa baada ya Taasisi ya SFO kushinda kesi, Tanzania tunarudi kufanya uchunguzi wa ndani kubaini hizo fedha dola milioni sita zilizoingizwa kwenye akaunti ya kampuni ya Egma na kutolewa zote muda mfupi zimekwenda wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu, ni nani,” alifafanua Balozi Sefue.
Balozi Sefue aliwataja wamiliki wa Egma kuwa ni aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Mitaji Tanzania, Fratern Mboya na Mkurugenzi Gasper Njuu.
Alitoa mwito kwa wamiliki hao, kutoa ushirikiano wakati wa uchunguzi wa sakata hilo na kwamba mara baada ya uchunguzi kukamilika, iwapo kutabainika makosa ya rushwa au mengine, sheria itachukua mkondo wake.
“Ombi letu na ombi la Rais John Magufuli watu hawa wanatakiwa kutoa ushirikiano na pengine ameongezeka mmiliki kwenye kampuni hiyo, wahakikishe wanatoa ushirikiano,” alisisitiza Balozi Sefue. Akizungumzia sakata hilo, Balozi Sefue alisema sio jambo geni kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari nchini vimeripoti jana, na kwamba tangu mwaka 2013, Tanzania inalifahamu na ndiyo iliyolipeleka SFO kuchunguzwa.
Akifafanua, alisema katika mwaka 2012/13, serikali ilifanya utaratibu wa kawaida unaofanywa na nchi mbalimbali duniani wa kukopa kwenye taasisi za benki ambapo Benki ya Standard ilikubali kuikopesha.
Alisema katika mkopo huo, serikali ilihitaji Dola za Marekani milioni 600 kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo kwa kawaida benki husika huingia mkataba na benki nyingine inayopewa jukumu la kutoa mkopo huo.
Alisema katika mchakato huo, Benki ya Standard kupitia kampuni tanzu iliipa Benki ya Stanbic Tanzania kazi hiyo ambapo fedha hizo zilipatikana na kwamba katika mchakato wa mkopo huo, ada ya mkopo serikali ilitozwa asilimia 2.4 ya mkopo.
Aliyataja masharti mengine kwamba yalikuwa ni kulipa mkopo riba kwa miaka saba, na kwamba deni hilo litalipwa kwa miaka saba, ambapo linapaswa kumalizika mwaka 2019. Balozi Sefue alifafanua kwamba baada ya mkopo kutolewa nusu ya kwanza, Mtendaji Mkuu wa benki hiyo wakati huo, Bashir Awale alikuwa na matatizo na watumishi, na Benki Kuu (BoT) iliingilia kati na kufanya uchunguzi.
Katika uchunguzi huo, kulibainika kasoro nyingi zikiwemo ulipaji wa fedha kwenye kampuni bila maelezo ikiwemo Kampuni ya Egma ambayo ilibainika kulipwa Dola za Marekani milioni sita.
Alisema fedha hizo zilionekana zimeingizwa kwenye Egma na kutolewa zote bila kutozwa kodi, ambapo katika taarifa yao ya ukaguzi, BoT ililionesha hilo na mambo mengine yaliyobaini na kumkabidhi Mwenyekiti wa Benki ya Stanbic Tanzania.
Hata hivyo, baada ya taarifa hiyo kupokewa, mwenyekiti wa benki hiyo aliitisha mkutano wa Bodi ya benki na waliipitia taarifa hiyo ya BoT na taarifa kupeleka Kitengo ya Uchunguzi cha Kimataifa cha Intelijensia.
Alisema katika uchunguzi huo, ndipo ilibainika kwamba nchi ilitozwa ada zaidi, ambapo ada ya mkopo halali ilikuwa Dola za Marekani milioni 1.4, lakini Stanbic walichukua Dola za Marekani milioni 2.4.
Alisema fedha hizo zilizoamriwa na Mahakama nchini Uingereza kwamba Benki ya Standard iilipe Tanzania ni zile ambazo hazikupaswa kuchukuliwa, ambazo ni dola milioni sita na dola milioni moja ni faida.
MAtokeo ya Michezo ya raundi ya pili ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia

MAtokeo ya Michezo ya raundi ya pili ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia

Matokeo ya Michezo ya raundi ya pili ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia

Matokeo  ya mechi zilizochezwa Jumanne ni kama ifuatavyo:
Cameroon 0-0 Niger (Jumla 3-0)
Congo 2-1 Ethiopia (Jumla 6-4)
Nigeria 2-0 Swaziland (Jumla 2-0)
Ghana 2-0 Comoro (Jumla 2-0)
Misri 4-0 Chad (Jumla 4-1)
Ivory Coast 3-0 Liberia (Jumla 4-0)
Tunisia 2-1 Mauritania (Jumla 4-2)
Afrika Kusini 1-0 Angola (Jumla 4-1)
Burkina Faso 2-0 Benin (Jumla 3-2)
Senegal 3-0 Madagascar (Jumla 5-2)
Mali 2-0 Botswana (Jumla 3-2)
Tanzania 0-7 Algeria(jumla 2-9)
Kenya 0-2 Cape Verde(jumla 1-2)