hekaheka za BVR Dar es Salaam


hekaheka za  BVR Dar es Salaam

  Dar es Salaam. Wakati uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, ukiingia siku ya tatu leo, kasoro lukuki zimeendelea kugubika mchakato huo huku katika baadhi ya vituo wananchi wakizichapa wakigombania kuingia chumba cha kujiandikisha.

Tukio la kutwangana makonde lilitokea katika Kituo cha Shule ya Mwangaza, Gongo la Mboto saa 2.15 asubuhi wakati uandikishaji ulipokuwa ukianza.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema: “Polisi unaowaona wamefika muda si mrefu, wala hawakuwepo hapa tangu asubuhi... ninadhani walipewa taarifa baada ya watu kuanza fujo wakigombania kuingia ndani  kujiandikisha,” alisema Magreth John na kuongeza:
“Watu wamepigana kwa sababu wanasema kuna wenzao ambao majina yao hayakuandikwa jana (juzi) halafu wamefika asubuhi wakaanza kuitwa ndani kujiandikisha. Hapo ndipo mzozo ulipoanzisha na ngumi zikafumuka.”
Msimamizi wa kituo hicho, Ramadhani Mshindo alisema mzozo huo ulitokea kwa sababu ya wananchi hao hawakuelewa utaratibu.
“Jana (juzi) jioni wakati tunafunga zoezi hili saa 12.00 jioni kuna watu wengi walikuwa kwenye foleni ambao hawakuandikishwa, kwa hiyo tuliwaandika majina ili leo (jana) wakifika hapa watangulie kuandikishwa kabla ya wengine. Sasa tulivyofika na kuanza kuita majina yao ili waingie kujiandikisha ndipo watu wakaanza fujo na kupigana ikabidi tupige simu polisi ili waje kutuliza ghasia,” alisema Mshindo.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Jica, Tabata wananchi walilalamikia suala la muda kwani waandikishaji walichelewa na hadi saa 4.30 asubuhi, asilimia kubwa ya watu hawakuwa wamepata huduma. “Nimefika hapa saa 12.00 asubuhi lakini hadi sasa sioni dalili ya kuandikishwa leo… Wametuambia wanaanza kuandikisha wale waliobaki jana kwa sababu majina yao yaliandikwa kwa hiyo sisi wa leo tunasubiri kwanza,” alisema Maria Saleh.
Maria alisema uandikishaji unakwenda taratibu kutoka na mashine kugoma mara kwa mara.
Malalamiko kama hayo yalitolewa na wananchi waliokuwa wamefika kujiandikisha katika Kituo cha Shule ya Msingi, Ulongoni, Gongo la Mboto na waandishi wetu walishuhudia watu wengi wakiwa kwenye misururu, wengine wakiwa wamelala pembeni ya kituo hicho baada ya kuchoka kusimama muda mrefu.
Hata hivyo, kwenye kituo hicho, wananchi walijiwekea utaratibu kwamba kila mtu anayefika anaandika namba kwenye daftari na kupewa kikaratasi kidogo chenye namba hiyo ndipo anapanga foleni.
Utaratibu ambao ulisaidia kupunguza usumbufu na kuondoa vuta ni kuvute wakati wa kuingia kwenye chumba cha kujiandikisha.
Lakini licha ya kujiweka utaratibu huo, Ibrahim Kitumbi alisema changamoto ya muda na vifaa ilikuwa palepale.
“Hivi tunavyozungumza watu waliyopewa namba wamefika 2,145. Hawa wameandika majina tu na kupewa namba. Waliojiandikisha tangu jana hawafiki hata 200. Sasa kwa siku nane zilizobaki kweli tunaweza kumaliza kuandikishwa! Huku si kutunyima haki?” alihoji.
Wakati wananchi wakitoa malalamiko hayo, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Ulongoni, Majura Mtalemwa alisema zoezi la uandikishaji linakwenda vizuri tofauti na wananchi wanavyolilalamikia.
Mkazi wa Temeke, Steven Almasi aliyefika kujiandikisha katika Kituo cha Magogoni, Yombo  alisema mwaka huu wa uchaguzi kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya wananchi kutoshiriki uchaguzi.
Mtendaji wa mtaa huo, Zeddy Zeddy alikiri kuwapo baadhi changamoto kwenye kituo chake ikiwamo uchache wa mashine za kuandikisha.
“Mwitiko wa watu umekuwa mkubwa tofauti na matarajio yetu kwa hiyo kama mashine zikiongezwa kwenye baadhi ya vituo, itasaidia kuondoa msongamano na kazi kukamilika kwa wakati,” alisema Zeddy.
“Kama Tume ingeongeza mashine, mambo yangekwenda vizuri zaidi lakini kinachoendelea ni ngumu kusema kuwa watu wote wataandikishwa kama ilivyopangwa,” alisema mtaalamu wa BVR aliyekuwapo Kituo cha Shule ya Msingi Kibangu, Ubungo, Suleiman Mahmoud.
Katika kituo cha Kontena – Tanesco, Kinondoni ni mashine moja tu iliyokuwa ikifanya kazi kati ya tatu kutokana na kuharibika licha ya idadi ya watu kuwa wachache.
“Mashine moja ilikuwa haifanyi kazi hadi saa tatu asubuhi, wameleta nyingine lakini nayo kamera inasumbua. Hii yangu printa haifanyi kazi hivyo ipo moja tu. Tumewapigia IT (mafundi wa Teknolojia ya Mawasiliano) wamesema wanakuja lakini wengi wanatembea kwa miguu wanachelewa kufika,” alisema mwendeshaji mashine ya BVR kituoni hapo, Max Phillipo.
Mkazi wa Mwananyamala, Hemed Shefaya alisema alifika kituoni tangu saa 10 alfajiri akiwa na wenzake watatu lakini kilifunguliwa saa 2.30 asubuhi.
“Mashine hizi zinaharibika mara kwa mara, kwa sasa wamezitengeneza lakini mikono ya wasimamizi ni mizito sana. Tulikuja jana na kupatiwa namba lakini hatukufanikiwa kuandikishwa… fikiria mimi namba 18 ya jana nimekuja saa 12 asubuhi lakini bado hadi sasa (saa 5.43) sijaandikishwa,” alisema Ramadhani Mkombozi aliyekuwa katika Kituo cha Shule ya Msingi Kisiwani, Mwananyamala.
Ofisa Uchaguzi wa Manispaa ya Kinondoni, Valence Urassa alisema tatizo la kuharibika kwa BVR lilikuwa likifanyiwa kazi na mafundi wa NEC na Manispaa na kwamba maeneo yenye wakazi wengi yalikuwa yakiongezwa mashine kufikia mbili kila kituo.
Kuhusu kuchelewesha kufungua vituo, alisema kituo chochote hakitafunguliwa 2.00 asubuhi iwapo waandikishaji hawatakuwa wamekamilisha maandalizi ya vifaa na kuandikisha kwani kuwahisha kutaleta matatizo.
Baadhi ya wasimamizi wametoa wito kwa NEC kuongeza vifaa pamoja na wataalamu ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.
Msimamizi wa Kituo cha Chuo cha Usafirishaji (NIT), Kelvin Donald alisema mashine alizonazo zinasumbua tangu juzi na hata baada ya kutoa taarifa na kubadilishiwa bado tatizo hilo linaendelea.
“Kwa wastani wanajitokeza watu 1,200 kila siku na hapa tuna mashine tano tu, moja haifanyi kazi,” alisema Donald.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Luis, Omari Mshauri alisema baada ya umeme kuwa kikwazo, juzi msamaria mmoja alijitolea jenereta huku wengine wakichangia mafuta kuendelea na kazi.
NEC yafafanua
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Malaba alisema wakazi wote wa jiji hili waliojitokeza wataandikishwa hata baada ya siku zilizopangwa kumalizika hivyo hawatakiwi kuwa na hofu.
“Hakuna mtu aliyejitokeza kuandikishwa halafu akaachwa… tutaandikisha mpaka wote waliojitokeza siku ya mwisho watakapokamilika.
“Mpaka sasa tuna mashine takriban 3,500 na nyingine zinaendelea kuingia kutoka mikoa ambayo tumeshakamilisha kuandikisha. Hizi zote zitaletwa kuongeza nguvu ya uandikishaji katika maeneo yenye wakazi wengi na kumaliza haraka,” alisema Malaba.
Kawe kujiandikisha upya
Malaba alieleza kuwa wakazi wa Jimbo la Kawe ambao walijiandikisha awali katika uandikishaji wa majaribio, watatakiwa kujiandikisha upya ili wapate vitambulisho vya sasa.
Hata hivyo, hakutaja sababu za kurudia na kuahidi kufafanua zaidi leo.
RC atoa maagizo
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amewataka wakurugenzi wote wa Manispaa za Dar es Salaam kutoka maofisini na kwenda kusimamia kwa karibu uandikishaji huo na kutatua matatizo yanayoripotiwa na wananchi kila wakati.
Alisema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, mojawapo likiwa waandikishaji kuchelewa kufika vituoni, kuwahi kuondoka kabla ya muda na mashine kugoma.
“Tutachukua hatua kali kwa ofisa mwandikishaji yeyote atakayekiuka taratibu na kukwamisha uandikishaji... tunafahamu uandikishaji unakabiliwa na changamoto nyingi, lakini nimepata taarifa kuwa waandikishaji pia wanahujumu uandikishaji bila sababu za msingi,” alisema Sadik.

Post a Comment

Previous Post Next Post