Magufuli apiga ‘marufuku’ mitambo ya kukodi

RAIS John Magufuli ametaka Shirika la Umeme Tanzania ( Tanesco) kuachana na miradi ya mitambo ya kukodi na kutosikia kuna mapendekezo ya kutaka kuongeza mkataba.
Amewataka watendaji wa shirika hilo kuondokana moja kwa moja na wazo la kufa kwa kuwasisitiza kwamba life mawazoni mwao huku akimhadharisha Waziri mwenye dhamana kwamba mtendaji atakayemshauri juu ya hilo, hafai, ikiwezekana amuondoe wizarani. Magufuli alisema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi II , jijini Dar es Salaam.
Alisema ipo mikataba mingi aliyoiita ya hovyo na kusisitiza kwamba Watanzania wamechoka na miradi ya hovyo ambayo kila siku imekuwa ikizaa matatizo. “Niwaombe Tanesco katika siku za usoni muachane na miradi ya kukodisha mitambo ya umeme na matumaini yangu sitasikia tena mnaleta mapendekezo kwamba mnataka kuongeza mkataba au tunataka kukodi,” alisema.
Akimsisitiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusimamia hilo, alisisitiza, “suala la kukodi likafe kabisa; na hayo mawazo nayo yakafe; kuwe na mawazo ya kujenga mitambo yetu.” Alisema lazima kuachana na umeme wa kukodisha usio na uhakika au wa kutumia watu. Alisema ndiyo maana kumekuwa na matatizo mengi kama ya IPTL .
Awafagilia Muhongo, Makonda Rais Magufuli ambaye ameeleza kufurahishwa na Wizara ya Nishati na Madini, aliitaka iende na kasi kubwa zaidi kwa kuachana na mitambo ya kukodi. Alisema nchi imechoka kufanyishwa biashara na wawekezaji aliowaita wa ajabu, kwa kulipia ‘capacity charge’ na bei za ajabu huku wakiumiza wananchi kwa bei juu. “Wizara endeleeni kujipanga vizuri kwa spidi ya hapa kazi tu na ndiyo maana niliamua kumrudisha Profesa Muhongo.
Na wakati mwingine vitu vizuri vinapigwa vita, hata Makonda (Paul-Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam) alikuwa anapigwa vita, nikaona mbaya wao nimrudishe hapa kwani kila nikisali naona Makonda anabaki hapa hapa,” alisema. Alisema hachagui mwanasiasa bali mchapakazi kwani maendeleo hayahitaji siasa. Alisema kila mmoja anahitaji maendeleo na ndiyo maana alichagua wachapa kazi.
Bwawa la Mtera Aidha aliwaambia Tanesco kwamba kutokana na mvua za mafuriko zilizotokea mkoani Iringa hivi karibuni, hatarajii kupewa taarifa za kupungua kwa maji kwenye bwawa la Mtera. “Kama mna mtindo la kufungulia maji na kusema maji ya Mtera hayatoshi kuzalisha umeme wakati tumeshuhudia watu wanapelekwa na maji, sitawaelewa,” alisema.
“Mkurugenzi (Felchesmi Mramba) sitakuelewa, Waziri (Muhongo) sitakuelewa na hata Katibu Mkuu (Profesa Justin Ntalikwa) sitakuelewa,”alisema Rais Magufuli. Alisema watakapoachia maji yakaondoka, wahakikishe umeme haupungui hata siku moja. Alisema ni lazima kuwaambia ukweli na kueleza kwamba anajua wamemwelewa. Alisema haiwezekani kuendelea kuwa masikini wakati wasomi wapo na wizara nzima ikiwa ina viongozi maprofesa.
Anayenikwamisha, atakwama Alisema serikali yake itafanya kazi kwani wananchi walimchagua bure bila kuwahonga kwa lengo la kuondoa kero. Alihakikishia umma wa watanzania kuwa amejipanga kufanya kazi na anayetaka kumkwamisha, atakwama yeye na kuondoka siku hiyohiyo. Aliwataka wananchi kusaidia serikali kwenda mbele kwa kufanya kazi na kuwapuuza wanaotaka kuchelewesha maendeleo.
Alisema upatikanaji wa umeme ni kipimo cha maendeleo ya nchi, hivyo bila kuwepo umeme wa uhakika ndoto ya kujenga uchumi wa viwanda haitakamilika. “Umeme ukiwepo, ndoto itakamilika na kujenga ajira kwa Watanzania,” alisema. Uzalishaji umeme Alisema uwezo wa nchi kuzalisha umeme ni megawati 1,200 hadi 1,500 kwa mwaka.
Alisema sasa uzalishaji umefikia megawati 1026 na kila Mtanzania anatumia wastani wa watt 30 kwa mwaka kiasi ambacho kiko chini licha ya kuwa na vyanzo vingi vya kuzalisha umeme. Alisema ikilinganishwa na nchi nyingine hususani Kenya, kila Mkenya anatumia watt 40, China watt 490 kwa mwaka, Afrika Kusini 500, Marekani watt 1,683.
Magufuli alisema kuweka jiwe hilo la msingi ni hatua nzuri kwani mradi utapunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la umeme. Alisema ndiyo maana baada ya kuingia serikalini na kukusanya mapato alihakikisha analipa dola milioni 120 ambazo ni asilimia 15 ya gharama za mradi zilizotakiwa kulipwa na serikali. Alisema katika gharama zote za dola za Marekani milioni 344, serikali ya Japan inatoa asilimia 85 ya gharama hiyo lakini Tanzania ilikaa miaka miwili kupata fedha hizo.
Alisema pia mtambo wa Kinyerezi I wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150 unaweza kuongeza na kufikia megawati 335 na mkandarasi anahitaji dola milioni 20 kuendeleza ujenzi na kuahidi kuzitafuta mwezi huu na kuanza ujenzi. Alitaka kampuni inayojenga mradi wa Kinyerezi II kumaliza mapema kama ilivyopangwa kwa ubora unaotakiwa kwa heshima ya fedha.
Akizungumzia ulipwaji fidia kwa wakazi wa Kinyerezi wanaodai Sh bilioni mbili, alisema atawapelekea fedha na kulipwa kwa mujibu wa sheria. Alitaka waliolipwa wasifanye ujanja kwa kuwa hakuna fedha za bure. Alisema mradi huo upo maeneo ya Kinyerezi ambako vijana na akinamama wanapaswa kupewa nafasi ya kupewa ajira.
Aliwataka wakipata ajira hizo wasiibe vifaa vya kazi kwani mradi ni wa Watanzania wote kwa kuwa wakiiba, itakuwa chanzo cha kuchelewesha mradi. “Ni vema kufanya kazi kwa ua minifu ili kuwanufaisha Watanzania wote kwani inatakiwa Tanzania mpya yenye maendeleo,” alisema. Aliwaeleza wakazi wa Kinyerezi kuwa katika mradi huo pia watajenga kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wa raia.
Aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa misaada yao na kuwathibitishia kuwa wataendelea kutoa ushirikiano na kuwahakikishia wadau wa maendeleo kuwa fedha walizotoa zitatumika kwa uangalifu bila kufuja na kupeleka panapotakiwa na kujenga nidhamu ya matumizi bora ya fedha. Umiliki Kinyerezi II Waziri Muhongo alisema mradi wa Kinyerezi II unamilikiwa na serikali kwa asilimia 100.
Serikali ya Japan imetoa Dola za Marekani milioni 292 ambao ni mkopo wa masharti nafuu na serikali imetoa dola za Marekani milioni 52 hivyo kutumia Dola milioni 344 sawa na Sh bilioni 740. Alisema tangu Rais Magufuli aingie madarakani, hali ya umeme imezidi kuimarika na kufikia megawati 1,000 ambazo hazijafikiwa ndani ya miaka mitano na kwa jana ilikuwa megawati 1,025 za mahitaji.
Alisema baada ya ujenzi wa mradi huo, utafuata wa Kinyerezi III wa megawati 600 na Kinyerezi IV megawati 330 na baadaye kuhamia mikoa mingine. Umeme wa mvuke Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mramba alisema mtambo huo wa Kinyerzi II ni wa kwanza kutumia teknolojia ya ‘combined cycle’ ambao umeme utazalishwa kwa gesi na pia kutumia mvuke.
Mradi huo utakuwa na mitambo sita ya Hitachi-25 itakayozalisha megawati 160 kutokana na gesi na mitambo miwili ya mvuke itakayozalisha megawati 80 na kufanya uzalishaji wa megawati 240. Alisema mitambo hiyo inatengenezwa na kampuni ya Hitachi ya Japan na itafungwa na mkandarasi wa Kampuni ya Sumitono ya nchini humo ikiwa ya kisasa yenye uwezo wa kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 20 ijayo

Post a Comment

Previous Post Next Post