Ndege yakamatwa ilikuwa ikisafilisha tumbili

WAKATI Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akiwasimamisha kazi mara moja wakurugenzi wanne na mameneja saba wa Kanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Idara ya Wanyamapori kutokana na usimamizi mbovu wa rasilimali za nchi, ndege iliyokuwa ikisafirisha tumbili 61 nje ya nchi imekamatwa.
Mbali ya ndege hiyo ya mizigo ya Afrika Kusini, serikali inawashikilia watu kadhaa kwa kosa la kutaka kusafirisha nyani hao, rubani wake na watu waliohusika kutoa vibali vya kusafirisha nyani hao kinyume cha sheria.
Aidha, Profesa Maghembe amesema magogo yenye thamani ya Sh milioni 500 yaliyokuwa yamekatwa katika msitu wa Kalambo wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa hivi karibuni, yametekezwa kwa moto na kuisababishia hasara serikali.
Waliosimamishwa kutoka TFS ni Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Juma Mgoo, Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Zawadi Mbwambo na Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Nurdin Chamuya huku aliyesimamishwa kutoka Idara ya Wanyamapori ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi.
Baada ya kuwasimamisha hao amewateua watu wengine kushika nafasi zao wakati mchakato wa kuwapata watendaji wapya ukifanyika na walioteuliwa kukaimu nafasi hizo ni Kaimu Mtendaji Mkuu TFS, Gerald Kamwendo, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Mwanaidi Kijazi, na Kaimu Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Haji Mpya na Kaimu Mkurugenzi upande wa Utawala, Emmanuel Winfred.
Profesa Maghembe alisema amewasimamisha kazi vigogo hao kwa kushindwa kusimamia na kudhibiti uvunaji haramu wa magogo, kusimamia ukusanyaji wa mapato na kushindwa kudhibiti usafirishaji wa wanyamapori.
Mbali na wakurugenzi hao, pia amewasimamisha kazi mameneja saba wa kanda wa TFS kwa kushindwa kusimamia ukusanyaji mapato yatokanayo na misitu katika maeneo yao.
Waliosimamishwa kazi na kanda zao katika mabano ni Hubert Haule (Kusini), Bakari Rashid (Mashariki), Cuthbert Mafipa (Kaskazini), Emmanuel Minja (Magharibi), Haji Khatibu (Ziwa) na Bruno Mallya (Nyanda za Juu Kusini).
Profesa Maghembe alisema amewasimamisha kazi maofisa hao kwa kushindwa kusimamia na kudhibiti uvunaji haramu wa magogo aina ya mkurungu na kusababisha uharibifu mkubwa katika Msitu wa Kalambo.
Jambo lingine ni ukusanyaji mapato ya serikali yatokanayo na misitu, lakini wakashindwa kuyapeleka benki na waliopeleka walipeleka kiwango kidogo kuliko walichokusanya na wengine hawakupeleka kabisa mapato hayo.
Kuhusu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Mulokozi, alisema amemsimamisha kazi kupisha uchunguzi kutokana na kutoa kibali cha kusafirisha nyani 61 kati ya 450 waliokamatwa katika maeneo mbalimbali ya Kilimanjaro na Arusha wakati alimpa maelekezo ya kutokutoa vibali hivyo kwa siku nane.
Mapato
Kuhusu mapato, alisema Januari mwaka huu aliagiza kufanyika ukaguzi wa makusanyo ya fedha, zilizotokana na mapato ya maliasili na namna mameneja wa TFS walivyoshiriki kukusanya fedha na kuziwasilisha serikalini.
Alisema Kamati iliundwa kuchunguza ukusanyaji wa mapato katika kanda mbalimbali. Alisema kamati hiyo ilibaini mapungufu makubwa na ilitoa mapendekezo ya kufanyiwa kazi.
“Kamati imepitia na wametoa maelekezo zichukuliwe hatua za kinidhamu mapema iwezekanavyo.Wale ambao wa kufukuzwa kazi wafukuzwe, wale wa kusimamishwa kazi na wasimamishwe na kushtakiwa na wale wa kupata makaripio makali wapate,” alisema Profesa Maghembe.
Aliongeza kuwa licha ya mapendekezo hayo, TFS haikuchukua hatua zozote juu ya watumishi hao. Waziri huyo alisema anaona biashara zinaendelea kama kawaida bila hatua zozote.
Magogo.
Alisema hivi karibuni walipokea taarifa ya uvunaji wa magogo katika msitu wa Kalambo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, William Ndile na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Magalula Magalula wakiomba msaada wa wizara juu ya udhibiti ilhali TFS ikiwa kimya.
Alisema baada ya taarifa hiyo, ilitumwa timu maalumu ya kuchunguza makosa makubwa kwenda kufanya uchunguzi.
Alisema timu hiyo iliona ni kweli magogo jamii ya mninga, yanakatwa na kutayarishwa huko huko na kisha kupakiwa katika makontena na kufungwa na rakili ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nyaraka zinatengenezwa Zambia kwa kuwa Tanzania hairuhusu kusafirisha magogo nje ya nchi.
“Kwa kuwa inajulikana sisi kwa sheria zetu hairuhusiwi kusafirisha magogo nje ya nchini, rakili inafungwa huko huko porini na nyaraka zinatoka Zambia na wakati mwingine makontena hayo hupitishiwa Zambia na kuingizwa nchini na kupitishwa hadi bandarini,” alibainisha Waziri.
Alisema yote hayo yalikuwa yakifanyika huku TFS wakifahamu juu ya uvunaji huo wa magogo, ambao Meneja wa Wilaya na Mkoa walikuwa na taarifa na hata yeye alipofika huko, alishuhudia uharibifu huo wa misitu.
Alisema kuwa aliagiza magogo hayo, yaliyopo msituni yatolewe msituni, yapelekwe Matai yaliko makao makuu ya wilaya kwa ajili ya kuyapiga mnada ili fedha zake zikasaidie shughuli nyingine za serikali kama kununua vifaa tiba.
Lakini baada ya wao kuondoka huko Machi 9, mwaka huu na kudhani kuwa magogo yote sasa yatakuwa yametolewa hadi Matai ili uandaliwe utaratibu wa kuyapiga mnada, ameambiwa kuwa magogo yale yamemwagiwa petroli na kuchomwa moto yakiwa na thamani ya Sh milioni 500.
“Kwa wiki mbili tangu tuagize magogo haya yawe yametolewa msituni, kama TFS wangechukua hatua haraka za kutoa magogo hayo, fedha za serikali zisingeweza kuchomwa moto na kukaa kuhangaika kupata fedha za kununulia dawa wananchi,” alieleza Profesa Maghembe.
Alisema kuna matatizo mengi katika TFS katika uvunaji wa misitu na wamekuwa wakifanya uchunguzi. Alisema kuna wavunaji misitu husafirisha mazao hayo kwa kutumia vivuli vya vibali, badala ya vibali halisi.
Maeneo mengine aliyoyasema yana matatizo ni katika vivuko vya ukaguzi, ambako alisema wapo watu ambao hawalipishwi ushuru kutokana na urafiki wao.
Hivyo alisema wamekubaliana na serikali, kubadilisha uongozi wa TFS ili kupata watu wengine, watakaoweza kusimamia vyema mapato ya serikali na rasilimali za misitu.
Nyani (tumbili)
Katika tukio lingine, Profesa Maghembe alisema juzi usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wamekamata watu wakitaka kusafirisha nyani ‘Velvety Monkey’ 61 kwenda nje ya nchi kwa kutumia ndege ya mizigo ya kukodi kutoka Afrika Kusini.
Alisema watu hao kutoka Ulaya Mashariki na washirika wao wa hapa nchini, walikodisha ndege ili kuwaondoa tumbili hao kwenda Ulaya Mashariki. Alisema harakati za kukamata tumbili hao porini zilianza wiki iliyopita na jumla ya idadi yao ni 450 ilhali kuna taasisi zinazolinda hayo mapori bila walinzi wa mapori hayo kujua.
Maghembe alisema tumbili hao walikamatwa kutoka Upare, Hanang, Manyara na Mlima Kilimanjaro na aliwaita wasimamizi na kuwapa taarifa juu ya watu hao, wanaokamata tumbili porini.
“Nikiwa Moshi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa nilimuita Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na kumuarifu juu ya kamata kamata hiyo na kumuagiza kutotoa kibali cha kusafirisha wanyama ili tuwakamate watu hao, lakini baadaye tukagundua yeye ndio amesaini kibali hicho kutoka Dar es Salaam,” alisema Maghembe.
Alisema watu hao hawakufuata taratibu, kwani hawakuwa na kibali cha kukamata wanyama hao na ofisi yake ina taarifa za kutokuwepo mtu aliyeomba kukamata.
Alimtaka Katibu Mkuu, Meja Jenerali Gaudence Milanzi kufanya uchunguzi wa kina tangu kukamatwa kwa twiga waliokuwa wakisafirishwa nje na waangalie wanaotoa vibali hivyo na wanaohusika na biashara ya wanyamapori.
Polisi yazungumza
Kwa upande wake, Polisi mkoani Kilimanjaro imesema imewakamata watu wawili raia wa Uholanzi kwa tuhuma za kusafirisha wanyamapori aina ya tumbili kupitia KIA; anaandika Arnold Swai kutoka Moshi.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema watu hao walikamatwa Machi 23, saa moja jioni, wakiwa katika uwanja wa Kia tayari kuwasafirisha wanyama hao.
Kamanda Mutafungwa alisema wanyama hao walikuwa 61 ambao walikuwa kwenye masanduku sita ya mbao na walikuwa wakisafirishwa kwenda Armenia kwa kutumia Kampuni ya Arusha Fright Limited. Alisema wanyama hao walikamatwa eneo la mizigo la CAGO na walikuwa wasafirishwe kwa ndege binafsi yenye namba EW/36 4G.
Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa ni Artem Vardanian (52) mwenye hati ya kusafiria namba NWF8CKJR8 na Edward Vardanian (46) mwenye hati ya kusafiria namba NY969P96, wote wakiwa ni raia wa Uholanzi.
Alisema watuhumiwa wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi KIA na wanyama wamehifadhiwa na uchunguzi unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Post a Comment

Previous Post Next Post