Rais wa Zanzibar achagua mawaziri 13

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ametangaza Baraza la Mawaziri lenye wizara 13.
Baraza hilo lina sura mpya nane, likiwajumuisha wajumbe kutoka katika vyama vya siasa vya upinzani, wanasiasa mashuhuri visiwani humo, huku naibu mawaziri saba wote wakiwa wageni katika nafasi hiyo.
Akitangaza majina hayo jana, Dk Shein anayeianza awamu ya pili ya utawala wake Zanzibar, alimtangaza Dk Halid Salum Mohammed, ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Donge, kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Katika awamu iliyopita, Dk Halid alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Riziki Pembe Juma, Mwakilishi wa Viti Maalumu, ameteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, wakati Moudin Castico, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi aliyeteuliwa na Rais, anakuwa Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto.
Wengine ni Rashid Ali Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Amani ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo.
Balozi Ali Karume, mmoja wa wanasiasa mashuhuri Zanzibar, ambaye kwa sasa ni Mwakilishi wa Kuteuliwa na Rais, yeye ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, huku Salama Aboud Talib, ambaye ni Mwakilishi wa Viti Maalumu na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake nchini (UWT), akiteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.
Balozi Amina Salum Ali aliyeshika nafasi ya pili, baada ya Rais John Magufuli, katika mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka jana, yeye ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko.
Wapinzani ndani
Dk Shein pia amemteua Hamad Rashid Mohammed, ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha ADC, ambaye pia amewahi kuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CUF, kuwa Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.
Hamad pia ndiye aliyeibuka katika nafasi ya pili katika Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Zanzibar kwa kupata kura 6,734 baada ya Rais Shein aliyeibuka na ushindi mnono wa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
Waziri huyo wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi alifuatiwa kwa karibu na mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyepata kura 6,076. Viongozi wengine kutoka vyama vya upinzani walioteuliwa katika Baraza la Mawaziri ni Said Soud Said kutoka AFP na Juma Ali Khatib kutoka TADEA, ambao wanakuwa mawaziri wasiokuwa na wizara maalumu.
Mawaziri wa zamani
Mawaziri wanaoendelea na nyadhifa zao ni Haji Omar Kheir aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali, huku Issa Haji Ussi Gavu ambaye katika kipindi kilichopita alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, amepanda na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Baraza la Mapinduzi.
Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi, Haroun Ali Suleiman, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Katiba, Sheria na Utawala Bora).
Mohammed Aboud Mohamed ambaye katika kipindi kilichopita alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, anaendelea na wadhifa wake huo bila ya mabadiliko, huku Mahmoud Thabit Kombo Jecha, ambaye ni Mwakilishi wa Kiembesamaki akipandishwa kutoka Naibu Waziri wa Afya kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.
Naibu Mawaziri Dk Shein ameteua naibu mawaziri saba wote wakiwa ni wapya akiwemo Lulu Msham Khamis kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Harusi Said Suleiman kuwa Naibu Waziri wa Afya.
Chum Kombo Khamis, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo na Mmanga Mjengo Mjawiri ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.
Wengine ni Juma Makungu Juma ambaye amechaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Maji, Ujenzi, Nishati na Mazingira, huku Khamis Juma Maalim, akiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na Mohammed Ahmed Salum akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.
Waliotemwa
Mawaziri waliotemwa ni pamoja na Dk Mwinyihaji Makame, Mwakilishi wa Dimani ambaye katika baraza lililopita alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee.
Mwingine ni Dk Sirra Umbwa Mamboya ambaye katika baraza lililopita alikuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili na katika Baraza la Wawakilishi alikuwa Mjumbe wa Kuteuliwa na Rais, ambaye mwaka huu hakupata uteuzi wowote.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Abdulhamid Yahya Mzee, Rais ataapisha mawaziri wapya na naibu mawaziri leo Jumapili Ikulu kwa ajili ya kuanza kutekeleza majukumu yao mapya kwa mujibu wa Katiba.
Lawama za SUK
Baada ya kutangaza mawaziri hao, Dk Shein alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa, imekwama kutokana na matakwa ya wananchi na si kikatiba.
Amefafanua kuwa tatizo ni vyama vya siasa ikiwemo CUF, kukacha kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio Machi 20, mwaka huu na kusisitiza hatishwi na uamuzi wa chama hicho na vingine vya upinzani kutoitambua Serikali yake.
“Kukwama kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa si kikatiba ni matakwa ya wananchi ambao waliamua kupigia Chama Cha Mapinduzi kura nyingi na kushinda katika majimbo yote ya uchaguzi Unguja na Pemba. “Tatizo hapa lipo kwa vyama vya siasa vilivyoamua kususia uchaguzi wa marudio ambao uliitishwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC,” alisema.
Dk Shein alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ameiongoza kwa miaka mitano, imetekeleza majukumu yake vizuri licha ya kuwepo kwa hitilafu ndogo ndogo alizoziita ni za kawaida.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo ya kukwama kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, iliyotokana na hatua ya makusudi ya CUF ya kutoshiriki katika uchaguzi wa marudio, Dk Shein amesema hatabadilisha vifungu vya Katiba kwa ajili ya kuruhusu na kutoa nafasi ya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyokuwa awali.
Kutambuliwa na Mungu
Alisema hababaishwi na kauli za CUF zilizotolewa na Maalim Seif za kutoitambua serikali yake na kusisitiza Serikali yake inatambuliwa na Mungu ambaye ameipa baraka zote pamoja na wananchi wa Unguja na Pemba ambao ndiyo walioipigia kura kwa wingi na kuipa nafasi ya kushika hatamu ya madaraka.
“Serikali yangu inatambuliwa na Mwenyezi Mungu kutokana na kudra zake na anayesema haitambui basi hiari yake, lakini mimi nawapongeza wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, ambao wamenipigia kura za ndiyo kwa ajili ya kunipa ridhaa ya kushika hatamu ya kuongoza dola,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post