Yanga vs TP Mazembe

KITENDAWILI cha makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) kiliteguliwa jana, ambapo wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo Yanga wamepangwa kundi moja na mabingwa wa zamani wa Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Upangaji wa ratiba hiyo ulifanyika jana mjini Cairo, Misri, ambapo TP Mazembe ni timu yenye umaarufu Tanzania, ambapo nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambaye kwa sasa anachezea KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta alitokea timu hiyo kabla ya kwenda Ulaya mwaka huu.
Pia Mazembe ni timu anayochezea Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu anayechezea pia Taifa Stars na tangu mwaka 2011 ilipokuja nchini kucheza na Simba katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ilitokea kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki.
Katika droo ya CAF jana mchana, Yanga imepangwa Kundi A na Mazembe, Mo Bejaia ya Algeria na Modeama ya Ghana na ratiba inaonesha mechi za makundi zitaanza Juni 17 mwaka huu. Kwa upande wa Kundi B zipo timu za Kawkab Athletic, Fath Union Sports zote za Morocco, Etoile du Sahel ya Tunisia na Ahly Tripoli ya Libya.
Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, Zesco ya Zambia imepangwa kundi moja na Al Ahly ya Misri, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Wac ya Morocco. Kundi B lina timu za Enyimba ya Nigeria, Zamalek ya Misri, Es Setif ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Yanga iliingia makundi ya michuano hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ambapo iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
Ilianza vizuri Ligi ya Mabingwa kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Wakati huo huo, awali jana Kamati ya Maandalizi ya michuano ya klabu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeiondoa AS Vita ya DRC kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kosa la kumtumia mchezaji Idrissa Traore hatua za awali akiwa anatumikia adhabu.
Kamati hiyo imefikia uamuzi huo katika kikao chake mjini Cairo, baada ya kupitia malalamiko ya klabu ya Stade Malien ya Mali dhidi ya As Vita juu ya Idrissa Traore.

Post a Comment

Previous Post Next Post