Mabasi ya haraka kuanza kutumia gesi




MSIMAMIZI wa Usambazaji Gesi katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Ismail Naleja, amesema awamu ya pili ya mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam yatatumia nishati ya gesi asilia badala ya mafuta jambo litakalosaidia kupunguza gharama. Katika awamu ya pili, mabasi mapya 200 ya mradi huo yanatarajiwa kuingizwa nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, kuhusu usambazwaji wa gesi katika magari, Naleja alisema hatua hiyo itaongeza idadi ya magari yanayotumia gesi nchini ambapo hivi sasa kuna mabasi 60 yanayotumia gesi na kuwashauri wenye magari kutumia mfumo huo ili kupunguza gharama za uendeshaji.
“Uendeshaji wa gesi utakuwa nafuu jambo linaloweza kufanya hata nauli zake kupungua kwani kilo moja ya gesi inatumika katika umbali unaotumiwa na mafuta ya dizeli lita moja na nusu,” alieleza Naleja.
Alisema kilo moja ya gesi ni Sh 1,500 wakati lita moja na nusu ni Sh 3,000, pia gesi haiharibu mazingira kwa sababu haina kaboni ikilinganishwa na petroli.
Aliongeza kuwa, gharama ya ufungaji wa mfumo wa gesi kwenye gari ni Sh milioni mbili, fedha ambayo inarudi baada ya kupunguza gharama katika matumizi kwa miezi mitano tu.
Mtaalamu huyo alisema matumizi ya gesi katika magari si hatari, kwani gesi inayotumika ni nyepesi kuliko inayotumika majumbani, hivyo ikivuja inasambaa hewani na tatizo likitokea mtungi wa gesi unajifunga.
Naye Msemaji wa Kampuni inayoendesha mabasi ya haraka ya UDART, Sabri Mabrouk alisema ni kweli kuwa awamu ya kwanza ya magari yaendayo haraka hayakuweza kutumia gesi kutokana na shirika hilo kuchelewa kupeleka wazo hilo. Hata hivyo sasa wameshafanya mazungumzo ili mradi wa awamu ya pili utumie gesi ili kupunguza gharama.
Alisema wanatarajia awamu ya pili ya mradi utakuwa na mabasi 200.

Post a Comment

Previous Post Next Post