TCU yashusha viwango kujiunga vyuo vikuu

TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), imetangaza kushusha viwango vya kujiunga na elimu ya juu (GPA) kwa wahitimu wa ngazi ya stashahada kutoka 3.5 hadi 3.0.
Bila kueleza sababu ya kufikia uamuzi huo, TCU imesema kushushwa kwa viwango hivyo kumelenga kuruhusu idadi kubwa ya wanafunzi kudahiliwa katika vyuo vikuu mbalimbali nchini, huku vigezo vingine vikisalia kama vilivyokuwa awali.
Pamoja na hilo, TCU pia imeongeza muda wa udahili kuanzia Septemba 12 hadi 23 mwaka huu ili kutoa fursa kwa waombaji wenye sifa kuchagua tena kozi zenye nafasi baada ya zile walizoomba awali kujaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Eleuther Mwageni, alisema jumla ya walioomba nafasi katika awamu ya kwanza ni 55,347.
Alisema katika awamu hiyo iliyohusisha wanafunzi kutoka kidato cha sita na wenye vyeti kutoka nje ya nchi jumla ya waliodahiliwa ni 30,731 ambapo kidato cha sita ni 30,529 huku wenye vyeti kutoka nje ya nchi wakiwa ni 202.
Waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza ni 24,616 ambapo 24,341 ni wale waliohitimu kidato cha sita na 275 ni wenye vyeti kutoka nje ya nchi.
Alisema katika jumla ya waombaji 55,347 walioomba wenye sifa za kudahiliwa ni 47,203 sawa na asilimia 85.3% waliopata ni 30,731 sawa na asilimia 65% waliokosa ni 16,472 sawa na asilimia 35% na wasiokuwa na sifa ni 8,144.
Mwageni alisema wengi waliokosa ni kutokana na kujaa kwa nafasi katika vyuo walivyoomba ambapo idadi kubwa ya waombaji kupendelea zaidi vyuo hivyo.
“Kwa mfano kozi zote zinazotolewa na Muhimbili na nyingi za Chuo cha Ardhi zimejaa, baadhi ya kozi zimekimbiliwa na waombaji wengi kuliko nafasi zilizopo katika vyuo hivyo,” alisema Mwageni.
Alizitaja kozi nyingine zilizojaa katika vyuo vilivyoombwa na idadi kubwa ya waombaji kuwa ni ualimu, udaktari wa binadamu, ufamasia, sayansi ya uthamini wa ardhi na sheria.
“Kozi ya ualimu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam ilikuwa na waombaji 15,803 wakati nafasi ni 1,000 tu. Halikadhalika kozi ya sayansi ya uthamini wa ardhi ya Chuo Kikuu Ardhi ilikuwa na waombaji 4,599 wakati nafasi ni 100,” alieleza Mwageni.
Aliongeza kuwa waliokosa nafasi ni kutokana na ushindani uliopo kutokana na uhaba wa nafasi katika kozi hizo huku baadhi ya waombaji wakishindwa kuzingatia sifa linganishi.
“Kwa hali hiyo Tume imeongeza muda wa udahili kuanzia Septemba 12 hadi 23 mwaka huu kwa waombaji wenye sifa ili wapate fursa ya kuchagua tena kozi zenye nafasi,” aliongeza Mwageni.
Mapema Julai mwaka huu, Tume hiyo ilitangaza kuongeza viwango vya kujiunga na elimu ya juu kwa wanafunzi waliohitimu ngazi ya stashahada kutoka  GPA 2.7 iliyokuwapo awali hadi 3.5.

Post a Comment

Previous Post Next Post