Ni binti,apiga A=32,B+=6 katika masomo 38, Amesoma shule za kawaida za serikali
Mhitimu bora wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2014, Doreen Kabuche
(22), aliushangaza umma uliohudhuria maafali ya 44 ya chuo hicho baada
ya kutangazwa kuwa kinara kwa ufaulu kwa kupata alama A 32 na B+ sita
kati ya masomo 38 ya shahada ya Takwimu Bima (Actuarial Science).
Kwa alama hizo, Doreen alipata wastani wa alama za ufaulu (GPA) 4.8 na
kuacha alama ya 0.2 ili kufikia kiwango cha juu kabisa cha ufaulu cha
alama tano, hivyo kupata shahada ya kwanza daraja la kwanza.
Akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum mwishoni mwa wiki, Doreen
anayeishi Kigogo Mwisho, jijini Dar es Salaam alihitimu shahada hiyo
akiwa miongoni mwa wanafunzi 28 wa darasa lake, lakini akihitimu
sambamba na wanafunzi wengine 5,745, wanawake wakiwa ni 2,298 wa shahada
ya kwanza.
Shahada hiyo inayotolewa katika Shule ya Sayansi ya Asili (CoNaS) chuoni
hapo, ni miongoni mwa taaluma adimu nchini. Ilianza kufundishwa chuoni
hapo mwaka 2011.
Miongoni mwa taasisi ambazo zitafurahia taaluma hiyo kuanza kupata
wataalam nchini ni pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo hulipa
fedha nyingi kupata huduma hiyo kwa wataalam kutoka nje ya nchi na kwa
gharama kubwa.
Alipopewa nafasi ya kuzungumza mbele ya mamia ya wanafunzi wenzake na
wageni waalikwa kwenye ukumbi wa Mlimani City, aliishia kutoa shukrani
kwa wahadhiri, wanafunzi wenzake na wote waliomsaidia katika mafanikio
yake kitaaluma.
Ili kupata wastani wa ufaulu wa daraja la kwanza kwa kiwango cha GPA ya
4.8, mhitimu hulazimika kufaulu kwa kiwango cha juu kwa miaka yote ya
kuwa chuoni. Doreen alifanikiwa kutimiza sharti hilo baada ya kufaulu
masomo 32 kwa kiwango cha ‘A’ na masomo mengine sita kufaulu kwa alama
za B+ kati ya masomo yote 38 ya shahada yake; baadhi ya yale
yaliyomkwamisha kupata A yakiwa ni ‘Actuarial Mathematics’ na ‘Legal
Matters in Actuarial Industry’.
Mgawanyo wa ufaulu wake kwa mwaka wa kwanza ulikuwa ni A za masomo 12 na
B+ za masomo mawili kati ya masomo 14; mwaka wa pili alifaulu kwa
kupata A katika masomo 10 na B+ mbili kati ya masomo 12 na mwaka wa tatu
alifaulu pia kwa kiwango cha alama A katika masomo 10 na masomo mengine
mawili akapata B+ kati ya masomo 12.
ALIKOTOKA
Tofauti na fikra za wengi kuwa siku hizi wanafunzi bora hutoka katika
shule zinazotoza ada kubwa na kutumia Kiingereza kama lugha kuu ya
mawasiliano, maarufu kama English medium’, Doreen anathibitisha kuwa
hilo halina ukweli.
Katika mahojiano na NIPASHE, alisema kuwa hajawahi kusoma katika shule
hizo zinazotoza ada kubwa za mamilioni ya fedha na badala yake, alipitia
katika shule za serikali kuanzia shule ya msingi mwaka 2004 hadi kidato
cha sita mwaka 2011.
“Shule nilizosoma kabla ya chuo kikuu ni Mlimani (Shule ya Msingi)
iliyopo Chuo Kikuu Dar es Salaam sehemu ya Mlimani, kidato cha kwanza
hadi cha nne nilimaliza katika sekondari ya Forodhani na kidato cha tano
na sita katika shule ya sekondari Benjamin Mkapa. Kote huko usafiri
wangu siku zote ni wa daladala.
“Na kama unavyojua, ni kugombana na makondakta kila asubuhi wakati wa
kupanda mabasi (daladala) kwenda shule na jioni wakati wa kurudi. Ila
yote hayo tumeyazoea na hivyo adha za usafiri hazikuwa tatizo kubwa,”
alisema Doreen na kuongeza:
“Juhudi, kujiamini na kuzingatia maelekezo ya walimu ni muhimu. Aina ya
shule ni nyongeza tu kwa sababu siyo wote wanaosoma shule hizo za
kitajiri wamekuwa wakifaulu. Wapo wanaofanya vizuri, na wapo wanaofeli
pia... ni kama ilivyo kwenye hizi shule zetu (shule za serikali).”
KINARA KIDATO CHA SITA
Mafanikio ya sasa ya Doreen hayakuja kwa bahati mbaya. Historia yake
inaonyesha kuwa kila hatua aliyopita alikuwa akifanya vizuri. Katika
matokeo yake ya kidato cha nne mwaka 2008, Doreen alifaulu kwa kiwango
cha daraja la kwanza akipata pointi tisa na kuchaguliwa kuendelea kidato
cha tano katika Shule ya Sekondari Benjamin William Mkapa baada ya
kuchagua mchepuo wa Uchumi, Hisabati na Jiografia (EGM).
Doreen aliendeleza makali yake katika mitihani yake ya kidato cha sita
baada ya kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza kwa pointi nne na kuwa
kinara wa mchepuo wa EGM Tanzania.
Kwa matokeo hayo, akapata nafasi ya kuwa miongoni mwa wanafunzi bora
Tanzania walioitwa bungeni mwaka 2011 na kutambulishwa na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, mbele ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kushangiliwa na wote waliokuwamo ukumbini.
“Hapo shauku yangu ya kutaka kuongeza juhudi zaidi na kufanikiwa kama
akina Migiro (Asha-Rose), akina Tibaijuka (Profesa Anna) na akina Spika
Anne Makinda ikaongezeka. Nikapania kufanya vizuri hadi chuoni na sasa
namshukuru Mungu kuwa hatua hiyo pia nimeivuka salama na kufanikiwa,”
alisema Doreen.
Pamoja na mafanikio yake kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, Doreen
alisema kuwa hajawahi kujihusisha sana na masomo ya ziada maarufu kwa
jina la tuition na badala yake, alitumia muda mwingi kujisomea,
kujadiliana na wanafunzi wenzake na mara kadhaa kusaidiwa masomo
nyumbani na mjomba wake Charles Mayalla wa Taasisi ya Teknolojia Dar es
Salaam (DIT).
Doreen alitangazwa kuongoza kwa ufaulu Chuo Kikuu Dar es Salaam ikiwa ni
siku chache tu baada ya msichana mwingine aitwaye Rachel Kiunsi wa
Shule ya Msingi Kimara 'B' jijini Dar es Salaam kuwa kinara wa somo la
Hisabati Tanzania baada ya kupata alama zote za somo hilo katika mithani
ya taifa ya darasa la saba.
MATARAJIO
Baada ya kumaliza shahada ya kwanza, matarajio ya sasa ya Doreen ni
kuendelea na masomo ya shahada ya uzamili (masters) ambayo hata hivyo,
anasema mchakato wake (kwa masomo ya Actuarial Science) ni ghali kwani
kabla ya kujiunga anatakiwa kufanya mitihani kadhaa kabla ya kuanza
shahada hiyo.
“Gharama za mithani hii ni kubwa. Kuna mitihani ya hatua nyingi hadi
kupata nafasi ya kuanza kusomea masters na gharama zake kwa ujumla
hufikia hadi Sh. milioni 10. Hizi ni gharama kubwa. Ila kwa sasa sijakaa
bure.
Wazazi wangu bado wananiunga mkono na mwenyewe pia nimejifunza kuwa
mpambanaji tangu wakati nikigombana na makonda ili kupanda daladala na
kuwahi shule,” alisema Doreen.
“Na hata sasa nimeshaanza mapambano ili kujiendeleza zaidi. Nimepata
kazi na fedha ninazopata nitaendelea kuzidunduliza kila mwezi ili
nitimize ndoto zangu. Hata kama nitalazimika kusubiri kwa mwaka na
zaidi, nitasubiri na mwishowe naamini kuwa Mungu ataniwezesha na
kufanikisha malengo,” alisema Doreen.
“Najua hata hawa kina (Prof.) Tibaijuka, Migiro na wengine hawakufika
walipo sasa kirahisi. Walipambana, na mimi pia ninapambana ili siku moja
kufikia level zao,” alisema Doreen.
WAZAZI, FAMILIA
Akiwaelezea wazazi wake, Doreen alisema kuwa baba yake (Kabuche) aliwahi
kuwa mfanyakazi wa benki kabla ya kuacha na kuwa mjasiriamali ambaye
hivi sasa yuko Mtwara. Mama yake aitwaye Janeth Kabuche pia ni
mjasiriamali.
Doreen alisema anawashukuru sana wazazi wake kwani mara zote wamekuwa
wakimsaidia kwa kila hali ili kutimiza malengo yake katika elimu.
Alisimulia kuwa hata alipotia fora kwa kutwaa zawadi za masomo yote
wakati wa mahafali ya kidato cha sita shuleni kwao Benjamin Mkapa mwaka
2011, wazazi wake walimtia moyo kwa kumnunulia kompyuta mpakato (laptop)
aina ya Dell.
“Kwetu nimezaliwa peke yangu. Nikishatulia na kuanza maisha yangu
binafsi baada ya kumaliza mambo ya masomo nitapenda kuwa na watoto wengi
ili kuongeza ukubwa wa familia... walau wafikie watoto saba hivi.”
DINI, MUZIKI, FILAMU
Licha ya kufanya vizuri katika masomo, Doreen huwa haachi kujihusisha na masuala mengine ya kijamii.
“Kila Jumapili huwa sikosi kwenda kwenye ibada katika kanisa letu la
Kigogo Luhanga. Vilevile mimi ni mpenzi wa muziki kama wa bendi ya Wazee
wa Ngwasuma (FM Academia), bongofleva na filamu pia huwa ninazitama...
(filamu) ninayoipenda inaitwa Think Like a Man, Act Like a Woman,”
alisema Doreen.
RATIBA AKIWA CHUONI
Doreen alisema kuwa wakati wote akiwa chuoni alizingatia ratiba kuu
aliyojiwekea kila uchao, ambayo ni kwenda darasani bila kukosa kipindi
chochote na baada ya hapo alikuwa hakosi majadiliano na wanafunzi
wenzake kama Catherine John na Shamim Nuah.
“Sikuwahi ku-dodge (kukacha) kipindi, sikuwahi pia kukosa discussion na
wenzangu bila sababu ya maana. Na siku moja moja za mwisho wa wiki
tulikuwa tukienda ku-refresh mind na wenzangu, hasa maeneo ya viwanja
vya Sinza na siku nyingine Mlimani City. Ila kila Jumapili ni lazima
kwenda kanisani pale chuo au kanisa la nyumbani kwetu Kigogo Luhanga,”
alisema Doreen.
Doreen ana ndoto za akufuata nyayo za kina Prof. Anna Tibaijuka, Dk.
Asha-Rose Migiro na Anne Makinda kwa kuwa ni miongoni mwa wanawake
waliofanikiwa katika medani za taaluma, uongozi na siasa.
No comments
Post a Comment