Header Ads

Header ADS

Rais Kikwete aongoza kumuaga Marehemu Komba Karimjee



RAIS Jakaya Kikwete jana ameongoza mamia ya wakazi wa Dar es Salaam waliojitokeza kuaga mwili wa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba aliyefariki Jumamosi jioni katika Hospitali ya TMJ ikielezwa kuwa kaondoka kama moto wa kiberiti.
Tukio hilo lilifanyika jana Dar es Salaam katika viwanja vya Karimjee, na kuwakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo Makamu wa Rais, Marais wastaafu akiwemo Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, mawaziri mbalimbali, manaibu mawaziri, viongozi wa vyama vya upinzani, mwanasheria mkuu, viongozi wa dini na wabunge.
Katika tukio hilo lililojaa simanzi na vilio vilitawala, huku baadhi ya nyimbo alizokuwa ameziimba marehemu, Kapteni Komba zikiimbwa na baadhi ya wasanii wakati wa kuaga.
Akizungumza katika tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda alisema msiba wa Kapteni Komba ni pigo lisilozibika kamwe na siku alipofariki alimpigia simu wakazungumza kwa saa nne kuhusu safari ya kamati hiyo kuelekea nchini Ethiopia kikazi.
Tulipanga mambo mengi yakiwemo namna tutakavyotekeleza majukumu na jinsi ya kwenda Ethiopia… wajumbe wa kamati ilikuwa waondoke Machi mosi…lakini saa kumi jioni nikapokea ujumbe kuwa Komba amefariki,” alisema Mtanda na kuongeza kuwa alikuwa amali na rasilimali kwa familia, Chama Cha Mapinduzi na hata kwa wananchi wake jimboni.
Alisema Kapteni Komba alisimamia haki za wazee na kwamba Kamati itaendelea kusimamia yote yaliyoasisiwa na Mbunge huyo wa Mbinga ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana alisema Kapteni Komba alikuwa muimarishaji na mkuzaji wa CCM katika maeneo mbalimbali kwa kupitia nyimbo zake.
Wakati wa msiba wa Nyerere atakumbukwa kwa ujasiri wake na msimamo wake kwani alitunga nyimbo nyingi zenye kuwaliwaza Watanzania,”alisema Kinana na kuongeza kuwa vishindo pamoja na sauti yake vimezimika.
Alisema kifo chake kimeleta pengo kubwa kwa CCM, wasanii huku daima akikumbukwa kwani wakati wa uhai wake aligusa maisha ya walio wengi akiwa mwanajeshi, mwalimu, msanii na hata mwanasiasa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama alisema serikali itaendelea kutekeleza mipango ya Maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa katika jimbo la Mbinga Magharibi kama ilivyokuwa imepangwa katika jimbo hilo.
Alisema Komba atakumbukwa kwa ucheshi, msimamo katika masuala mbalimbali pia mchango wake kupitia vipaji alivyokuwa navyo.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema kifo cha Komba kaondoka na moto wa kiberiti, akiondoka na talanta zake, jambo linalosababisha wengi kutokuamini ambapo Mungu haachi kutoa mafundisho.
Alisema Kapteni Komba ilikuwa aende nchini Ethiopia na wenzake na kabla ya mauti kumkuta alikuwa akiandika nyimbo.
Kifo kitampata kila yeyote…angejua na kupewa hata muda kidogo angesema wale wote waliomkosea anaomba wamsamehe…na pia sisi tunapaswa kumsamehe,” alisema Makinda na kuongeza kuwa wakati mwingine watu hutumia midomo isivyo na ikumbukwe kuwa kila mmoja anatoka kwa Mungu.
Alisema Kapteni Komba alitekeleza wajibu wake kama binadamu na amekwenda kupeleka hesabu yake ya aliyoyafanya duniani huku CCM ikiamini kuwa Mungu atawapa Mbunge mwingine katika jimbo hilo.
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, aliyewakilishwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari alisema pamoja na itikadi zao bungeni lakini umoja wao ni nguzo kuu.
Alisema kifo ni safari ya kila mmoja, na kila binadamu anapaswa kutambua kuwa maisha ni mafupi na kujifunza kutenda mema kuanzia ngazi ya familia na hata kwa taifa.
Mweyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema Kapteni Komba alikuwa na utendaji ulio bora alifanya hivyo bungeni akiwa na uwezo wa kusimanga viongozi bila kuwaudhi.
Alisema alikuwa mkweli akistahili kukumbukwa kwa uongozi alioutoa kupitia kipaji chake cha kuimba na baadaye katika Bunge na zaidi katika kusaidia CCM.

No comments

Powered by Blogger.