Mabasi Yaendayo Haraka kuanza kazi oktoba 2
HATIMAYE mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika jiji la Dar es Salaam unatarajiwa kuanza Oktoba 2 mwaka huu kwa njia moja.
Aidha, wamiliki wa magari, pikipiki na baiskeli ambao watakutwa wakitumia barabara ya mabasi ya haraka, kama maegesho watapewa adhabu kali ya faini au kifungo gerezani.
Hayo yalibainishwa jana na Ofisa wa Fidia wa Wakala wa Usafiri Haraka wa Mabasi (DART), Deo Mutasingwa baada ya wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kufanya ziara ya kujionea jinsi huduma hiyo itakavyotolewa.
Alisema huduma hiyo ambayo ni ya muda na kufanywa kwa kipindi cha miaka mwili, itakayofanywa na Kampuni ya UDA, itaanza Oktoba 2 mwaka huu kwanjia moja ya kutoka Kimara hadi Kivukoni yenye urefu wa kilomita 20.9.
Alisema kwa njia za barabara ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi eneo la makutano ya Morocco jijini Dar es Salaam, itaanza kutumika baada ya miundombinu yake kukamilika.
Alisema katika mradi huo wa muda wa miaka miwili, mabasi 100 yatakayoendeshwa na madereva 200 yanatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo.
Aidha, Mutasingwa alisema wenye magari, pikipiki baiskeli ambao watakutwa wakitumia barabara hizo au kuegesha vyombo vyao watatozwa faini ya kati ya sh 250,000 hadi sh 300,000 au kifungo cha miaka miwili jela au adhabu zote kwa pamoja.
“ Tumekuwa na changamoto kwa watumiaji wengine wa barabara, jambo ambalo linaleta uharibifu na pia kuingilia safari. Tumeshazungumza na wenzetu wa halmashauri kushughulikia hili, hivyo kuanzia mwezi ujao atakayekutwa akitumia barabara hizo au kupaki chombo chake adhabu kali itakuwa juu yake,” alisema.
Alipoulizwa suala la nauli, alisema hilo liko kwenye mchakato kati ya DART, wamiliki wa mabasi na walaji lengo ni kuja na nauli ambayo haitamuumiza mwananchi lakini pia yule anayeendesha apate faida.
Alisema wakati utoaji wa huduma hiyo utakapokuwa kamili, watanzania takribani 300,000 watahudumiwa kwa siku.
Msimamizi wa Mifumo wa DART, Junn Mlingi alisema vituo vikuu vya mabasi vitakuwa na miundombinu ya kumwezesha mtumiaji yeyote kama ni mgeni, mlemavu wa viungo kuona au kusikia kuweza kupata huduma hiyokwani kutakuwa na matangazo ya sauti na maandishi.
Alisema mabasi hayo yatakuwa yakiendeshwa kwa kilomita 50 kwa saa kwa mwendo wa kasi na kilomita 24 kwa saa kwa mwendo wa wastani.“
No comments
Post a Comment