Header Ads

Header ADS

Kesi za mafisadi kutozidi miezi 9

JAJI Mkuu, Mohammed Chande Othman, amesema Mahakama Maalumu ya Uhujumu Uchumi na Ufisadi itaamua kesi kwa muda usiozidi miezi tisa na kwamba itaanza na majaji 14.
Aidha, wameandaa kozi maalumu kwa majaji 14 watakaofanya kazi katika mahakama hiyo itakayoanza Julai 11 hadi 15, mwaka huu, kwenye Chuo cha Mahakama Lushoto mkoani Tanga, ili kupeana mwongozo juu ya uendeshaji wa mahakama hiyo.
Jaji Mkuu alisema, kesi zitakazoendeshwa katika mahakama hiyo ni zile ambazo upelelezi wake umekamilika ili uamuzi utolewe mapema. Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupambana na uhalifu huo.
Aliyasema hayo jana wakati alipotembelea Maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, ambayo alisema yamezidi kuwa bora kuliko miaka mingine. Alisema baada ya sheria hiyo ya uhujumu uchumi kupitishwa na Bunge, imekuwa na marekebisho mengi na kuboreshwa kwa kiasi kikubwa.
Jaji Mkuu alisema pia, hatua inayofuata ni Rais kutoa idhini ya sheria hiyo na baadaye kupitishwa kwa kutangazwa katika Gazeti la Serikali ili ianze kutumika.
Alieleza kuwa baada ya kutangazwa katika Gazeti hilo la Serikali, Jaji anatakiwa kutunga kanuni mbalimbali, mojawapo ikiwa ya kulinda mashahidi kutokana na kuwa sheria hiyo inahusu makosa makubwa na hatari ya ugaidi, rushwa na uhujumu uchumi.
“Tuko mbioni kutunga kanuni hizo na kuhakikisha mashahidi wanalindwa. Jengo la mahakama hii litakuwa katika Chuo cha Sheria karibu na Mlimani City na tayari tumepeleka wasajili watendaji,” alisema.
Mwishoni mwa wiki, Jaji Mkuu huyo alisema kuwa majengo ya mahakama hiyo yatakabidhiwa leo. Kutokana na maelezo yake, Mahakama iko tayari kuendesha divisheni hiyo, baada ya kukabidhiwa majengo hayo.
Alisema wataanza kutoa semina kwa majaji na watumishi wengine wa mahakama hiyo juu ya namna divisheni hiyo itakavyoendesha shughuli zake. Aidha, aliweka wazi kuwa hadi sasa hakuna kesi hata moja iliyokwishatambuliwa kwamba itashughulikiwa na mahakama hiyo.

No comments

Powered by Blogger.