Agizo la Magufuli kwa MaRC mwisho leo

SIKU 15 alizotoa Rais John Magufuli kwa wakuu wa mikoa, wawe wamejumlisha wafanyakazi wote na kuhakikisha wanaondoa wafanyakazi hewa, zimetimia leo. Baadhi ya mikoa imeanika idadi ya watumishi hewa, waliobainika kupitia uhakiki huo, lakini mingi haijafanya hivyo.
Agizo hilo la Rais Magufuli ni sehemu ya maagizo kadhaa aliyotoa Machi 15 mwaka huu wakati akiwaapisha wakuu hao wa mikoa jijini Dar es Salaam; ambao aliwasisitiza kuwa ili mradi wamekubali kushika wadhifa huo, wameingia kwenye mtego.
Pamoja na majukumu mengine waliyopewa kuhakikisha wanayatekeleza katika uongozi wao, suala la watumishi hewa ni mtego unaowakabili wakuu hao wa mikoa wakipaswa kujinasua nao ndani ya wiki hii ambao siku zilizotolewa zimefika ukomo; Vinginevyo, wataweka rehani nyadhifa zao.
Majukumu mengine ambayo wakuu hao wa mikoa walipewa na Rais wahakikishe wanayatekeleza, ni pamoja na kukabili ujambazi hususan wakuu wa mikoa ya pembezoni inayokabiliwa na tatizo la utekaji magari kiasi cha serikali kuamua kuweka utaratibu wa polisi kuyasindikiza.
Mengine ni kukabili watu wazembe, watendaji wanaowanyanyasa wananchi, njaa, kodi za mazao, migogoro ya ardhi na kuhakikisha wanasimamia mpango wa elimu bure unafanikiwa.
Tangu Rais atoe maelekezo hayo ya kukabili wafanyakazi hewa, mikoa mbalimbali inaendelea na mchakato wa kuhakiki wafanyakazi kwenye idara na taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwataka watumishi kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwemo barua za ajira.
Katika mchakato huo ambao umezaa matunda kwa kubaini watumishi hewa waliokuwa wakilipwa mishahara, baadhi ya halmashauri zililazimika kufuta huku baadhi ya halmashauri zimeamuru watumishi wake walio masomoni na kwenye likizo, warudi mara moja katika vituo vyao vya kazi kuhakikiwa.
Madudu yaibuliwa Miongoni mwa mikoa ambayo imetoa taarifa za uhakiki ni pamoja na mkoa wa Dodoma, ambao umetajwa kuwa na watumishi hewa 144. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, ameagiza kupelekewa orodha ya watumishi hao na wakati huo huo kupatiwa maelezo kwa nini kuna watumishi hewa na kutaka kupatiwa orodha za watumishi hao.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa aliyehamia Mkoa wa Songwe, Rugimbana alisema uhakiki wa watumishi wa serikali umebaini uwepo wa idadi hiyo ya watumishi hewa .
Mkoa wa Kigoma pia ni miongoni mwa mikoa ambayo taarifa zake za uhakiki zimeshatolewa ambako imebainika kuwapo watumishi hewa 169 kwa kipindi cha mwaka uliopita.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emanuel Maganga amewataka wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote waliopo katika halmashauri zote kutaja kiasi cha fedha kilichotumika kulipa mishahara watumishi hewa hao 169 ndani ya kipindi hicho cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo wa Kigoma, watumishi hewa waliowabaini, wamo waliokwishafukuzwa, waliofariki na wengine wasiokuwa na sifa za kuwa watumishi wa umma.
Maganga ametaka fedha walizokuwa wakilipwa watumishi hao hewa kwa ajili ya mishahara, zirudi na wakati huo huo wakurugenzi wawafute kwenye orodha ya malipo.
Halmashauri za mkoa wa Kigoma zenye watumishi hewa na idadi yake kwenye mabano ni Kasulu (78), Kigoma (23), Manispaa ya Kigoma Ujiji (29), Buhigwe (11), Uvinza (19), Kibondo (5) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa yenye watumishi hewa wanne.
Halmashauri ya Kakonko ndiyo pekee isiyo na mtumishi hewa. Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, alisema leo ambayo ndiyo ukomo wa muda aliotoa Rais, atatoa taarifa kamili ya kazi hiyo ya kuhakiki wafanyakazi na kuondoa wafanyakazi hewa watakaokuwa wamebainika.
Ndikilo alisema, ipo timu inayo endelea kufanya uhakiki kwenye wilaya mbalimbali kwa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri. Likizo zaahirishwa Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam, Halmashauri ya wilaya ya Temeke ililazimika kuwaita watumishi wake walioko masomoni na likizo kurudi mara moja katika vituo vyao vya kazi wahakikiwe.
Msemaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Joyce Nsumba alisema hivi karibuni uhakiki uliendelea kwa makundi mbalimbali wakiwemo watumishi kutoka Idara ya Afya, Elimu, Fedha na Biashara, Kilimo, Mifugo, Ujenzi na Maendeleo ya Jamii.
Wakati anazungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Nsumba alisema walishahakiki watumishi 8,000. Sababu za uhakiki Uamuzi wa Rais Magufuli kuamuru ufanyike uhakiki, ulitokana na uchunguzi uliofanywa katika mikoa ya Singida na Dodoma katika halmashauri 14 na kugundulika kwa watumishi hewa 202 wanaolipwa mishahara.
Aliagiza uhakiki kwa watumishi wote katika wizara, mikoa, wilaya, idara,taasisi na Wakala za Serikali ndani ya siku 15. “Sasa niwaombe ndugu zangu wakuu wa mikoa, najua mtakwenda kuwapa maagizo wakurugenzi na wakuu wa wilaya.
Lakini niwape muda, ndani ya siku 15, wawe wamejumlisha wafanyakazi wote, wamewatoa wafanyakazi hewa,” ali waagiza. Rais Magufuli alisema mshahara ujao, ikigundulika kuwapo wafanyakazi hewa kwenye orodha ya malipo, mkurugenzi husika ajihesabu hana kazi na atafikishwa mahakamani.
Vile vile amewaambia mawaziri, hususan Waziri wa Fedha na Mipango aliyekuwapo kwenye hafla hiyo, wakawaeleze watendaji kwenye wizara zao na taasisi mbalimbali wahakikishe wanawaondoa wafanyakazi hewa ndani ya siku 15 na wasipotimiza agizo hilo hatua zitakuwa ni zilezile kwani sheria ni msumeno.
Alisema inasikitisha kuona fedha zinazokusanywa haziendi kwenye miradi inayopangwa, badala yake sehemu kubwa inatumika kulipa mishahara ikiwemo hewa. Alisema kwa ujumla Serikali inalipa mishahara kila mwezi kwa watumishi wake wa umma jumla ya Sh bilioni 549 mpaka bilioni 550.
Alisema kwa hali ilivyo, fedha nyingi zinaishia kwenye mishahara feki. Nawapa Ma-RC siku 15 mhakikishe Wakurugenzi wa halmashauri zote wamejumlisha idadi ya wafanyakazi wote waliopo na kuondoa wafanyakazi hewa katika halmashauri zao,” alisisitiza Rais Magufuli.
Mikoa ya Tanzania Bara ni: Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida, Tabora, Pwani, Manyara, Mara, Morogoro na Kilimanjaro

Post a Comment

Previous Post Next Post