Kuapisha kwa rais wa zanzibar

RAIS Ali Mohammed Shein ameapa kuiongoza tena Zanzibar huku akiahidi kuunda serikali itakayowaunganisha Wazanzibari wote.
Uundwaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ni jambo linalosubiriwa kwa hamu na wananchi, kuona kama Dk Shein baada ya kushinda kwa zaidi ya asilimia 90, ataunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hiyo ni kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) ambacho ni chama kikuu cha upinzani, kususia uchaguzi wa marudio uliompa ushindi wa kishindo Dk Shein kwa kile wanachodai kuwa hawawezi kushiriki uchaguzi haramu ambao matokeo yake ni kubakwa kwa demokrasia.
Lakini Dk Shein wakati amemaliza kuapa na kusomewa dua na viongozi mbalimbali wa dini kutoka madhehebu ya Kiislamu, Wakatoliki na Anglikana kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja jana, aliwahakikishia Wazanzibari kuwa ataendelea kuulinda umoja wao kwa kushirikiana na vyama vya upinzani ili kuiletea Zanzibar maendeleo.
“Vyama vya upinzani vimenipa imani kubwa hasa kutokana na maelezo yao waliyoyatoa siku ya kutangazwa matokeo, ujumbe wao ni wa kuijenga Zanzibar na mimi naahidi kuwa nitashirikiana nao bila ubaguzi wowote,” alisema Dk Shein anayeongoza muhula wake wa pili na wa mwisho kikatiba.
Alisema serikali atakayoiunda itaheshimu misingi ya utawala bora, haki za binadamu na hivyo aliwaomba wananchi wamuunge mkono kwa kufanya kazi ili wajiletee maendeleo kwa kuwa uchaguzi tayari umeshaisha.
“Uchaguzi umeisha, sasa tushirikiane wote kuijenga Zanzibar yetu, kila mtu akafanye kazi maana kila mtu mchango wake ni muhimu kwa ustawi wa nchi yetu,” alisema Dk Shein.
Pia alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kuitunza amani iliyopo huku akionya kuwa serikali yake ile ya Muungano haitakuwa na uvumilivu kwa mtu au kikundi kitakachojaribu kuvuruga amani iliyopo.
Hata hivyo, aliahidi kutoa mwelekeo wa Serikali yake atakapokuwa anazindua Baraza la Mapinduzi Zanzibar hivi karibuni. Hali ilivyokuwa Amaan Jina la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha ndilo lililoshangiliwa kwa nguvu na wafuasi wa CCM waliofurika kwenye Uwanja wa Amaan wakati wa shughuli ya kumwapisha Dk Shein.
Jecha aliyejitokeza akiwa kwenye jopo la watu mashuhuri ambao waliitwa kwenda kwenye jukwaa maalumu, lililoandaliwa kwa ajili ya Rais Mteule kuapa, alishangiliwa kwa nguvu wakati anashuka kwenda jukwaa hilo.
Jopo hilo lilihusisha Spika wa Baraza la Wawakilishi, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Katibu Kiongozi, viongozi wa dini pamoja na viongozi wengine liliongozwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu.
“Jecha, Jecha, Jecha,” wananchi waliimba jina hilo mara kwa mara wakati anaenda kwenye jukwaa hilo na wakati wanarudi baada ya kumaliza shughuli za kumwapisha Rais Shein. Jina la Jecha limekuwa maarufu baada ya kutangaza kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.
Tangu atoe tangazo hilo, hawakuwahi kuonekana hadharani hadi juzi alipojitokeza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa marudio. Kufutwa kwa uchaguzi huo, kumefanya kuwepo na mpasuko mkubwa wa kisiasa visiwani hapa baada ya CUF ambacho ni chama kikuu cha upinzani kutangaza kususia kushiriki marudio ya uchaguzi uliofanyika Machi 20, 2016.
Maelfu ya watu walifurika katika uwanja wa Aman kushuhudia tukio hilo la kihistoria, lakini kwa bahati mbaya zaidi wengi wa watu hawakupata nafasi ya kuingia ndani na hivyo kulazimika kubaki nje na kusikiliza sherehe hizo kupitia vipaza sauti vilivyofungwa uwanjani hapo.
Kikundi cha Culture kilikuwepo kutumbuiza sherehe hizo. Nyimbo zake za ‘aliyepewa kapewa, hapokonyeki, hata ukifanya chuki unajisumbua’ na ule wa ‘unaomba radhi ya nini wakati uliyokusudia hayakuwa’, zilipamba sherehe hizo na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi.
Sherehe hizo pia zilipambwa na gwaride la vikosi vya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Mafunzo na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).
Vikosi hivyo vilichora herufi ya A ambacho ni kifupi cha neno la Kigiriki la Alfa, ambalo maana yake ni mwanzo. Kuapishwa kwa Dk Shein jana ni mwanzo wa kuiongoza Zanzibar kwa muhula wa pili akiwa Rais wa Awamu ya Saba ya Zanzibar.
Marais wengine waliowahi kuiongoza Zanzibar tangu Mapinduzi ya mwaka 1964 ni Abeid Amani Karume, Aboud Jumbe, Ali Hassan Mwinyi, Abdul Wakil, Salmin Amour na Amani Abeid Karume.

Post a Comment

Previous Post Next Post