Asha-Rose Migiro ni moja kati ya waliochukua
fomu ya kuomba ridhaa ya Chama cha
Mapinduzi ya kupitishwa kugombea nafasi ya
Urais katika uchaguzi mkuu mwezi oktoba
kupitia tiketi ya chama hicho.
Migiro ni miongoni mwa waliotajwa tano bora
za urais CCM
Ingawa hakuwa akitajwa mara kwa mara
kwamba ni mmoja wa wagombea tishio,
kupitishwa kwa jina la Dk Asha-Rose Migiro
kuingia katika tano bora ya kuwania urais
kwa tiketi ya CCM, siyo jambo la ajabu.
Rekodi yake kitaifa na kimataifa lakini pia
jinsia, ni mambo ambayo yamechangia kwa
kiasi kikubwa Waziri huyo wa Katiba na
Sheria, kuvuka hatua hiyo ya kwanza.
Dk Migiro ambaye pia ni Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa, Idara ya Siasa
na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM, alijitosa
katika safari ya kuelekea Ikulu Juni 15 pasi
na mbwembwe za aina yoyote.
Mtanzania huyo ambaye aliweka rekodi ya
kuwa Mwafrika wa kwanza mwanamke
kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa (UN), alikuwa akitajwa kuwa
anaweza kuwa mwanamke wa kwanza
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Hakuwahi kutangaza nia kama ilivyokuwa
kwa makada wengine waliotumia fursa
hiyo kuelezea mikakati yao lakini pia,
hakuwa na mbwembwe katika kutimiza
sharti la kusaka wadhamini mambo
ambayo pengine yalimwongezea sifa za
kupitishwa miongoni mwa wagombea 38
waliokuwa wamechukua na kurejesha fomu
kuomba nafasi hiyo ya juu kabisa katika
utawala wa nchi.
Lakini kigezo kingine kilichomvusha ni
umakini wake na kutokulengwa na mishale
ya kashfa ambazo ziliwakumba mawaziri
kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Tano
na yote hayo yanampa fursa kubwa ya
kufika mbali katika safari yake hiyo hasa
ikiwa hoja ya nafasi ya wanawake kushika
urais kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa
Spika wa Bunge la 10 itatiliwa maanani.
Dk Migiro alianza kutajwatajwa miongoni
mwa wanaoweza kumrithi Rais Jakaya
Kikwete baada ya kumaliza mkataba wake
Umoja wa Mataifa na kurejea nchini na
mara moja kuteuliwa kuwa mbunge na
Waziri wa Katiba na Sheria.
Msimamo wake
Wakati akizunguka katika mikoa
mbalimbali kusaka saini za wadhamini, Dk
Migiro alikuwa makini katika kuzungumza
huku akisisitiza kuwa anasubiri Ilani ya
CCM... “Na mimi nitaweka mikakati ya
kuendeleza yale ambayo yameshafanyika.
Sasa endapo nitapata ridhaa ya chama
changu, nyenzo yangu kuu itakuwa ni Ilani
ya Uchaguzi ya CCM.”
Alisema kwa kuwa uchumi umeendelea
kukua awamu hadi awamu, naye
atahakikisha kukua huko kunawafikia
wananchi wengi zaidi: “Nitahakikisha kuwa
mambo haya yaliyofanywa na awamu za
uongozi zilizopita yanakuwa stahamilivu
na endelevu na kuwafikia wananchi walio
wengi zaidi.”
January Makamba ni moja kati ya waliochukua
fomu ya kuomba ridhaa ya Chama cha
Mapinduzi ya kupitishwa kugombea nafasi ya
Urais katika uchaguzi mkuu mwezi oktoba
kupitia tiketi ya chama hicho.
January ni miongoni mwa waliotajwa tano bora
za urais CCM
Alijiandaa na haikushangaza kusikia akiwa
miongoni mwa wagombea watano
waliovuka katika mchujo wa Kamati Kuu
(CC) na kuingia katika hatua ya kupigiwa
kura na Halmashauri Kuu (NEC).
Tangu alipotangaza nia, January Makamba
(41), amekuwa katika hekaheka za
kujitangaza na kujinadi siyo kwa wanaCCM
pekee, bali hata wananchi kupitia
machapisho mbalimbali.
Hata hivyo, hadi mwaka 2012, Naibu
Waziri huyo wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, hakuwa na mipango ya
kugombea urais. Aliwahi kuhojiwa katika
kipindi cha mikasi cha Televisheni ya EATV
na kusema hana mpango huo kabisa.
Pengine Mbunge huyo wa Bumbuli alikuwa
na lake moyoni kwani Julai 2, mwaka jana
aliweka bayana nia yake wakati
alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC
na kusema atagombea urais kwa sababu
Tanzania inamhitaji mtu mwenye sifa kama
zake, wa kizazi cha sasa.
Tangu wakati huo, January amefanya
mambo mengi ya kujizatiti kwenye nia yake
hiyo ikiwamo kutoa kitabu maalumu cha
maswali 40, kilichoandikwa na mwandishi
Privatus Karugendo kikionyesha kikijibu
maswali mbalimbali kuhusu namna
mwanasiasa huyo kijana atakavyoweza
kupambana na changamoto za urais iwapo
chama chake kitampa ridhaa na
Watanzania wakamchagua.
Wakati akiendelea na harakati zake
Februari, 2014 yaliibuka mambo
yasiyotarajiwa baada ya vikao vya CCM
kutoa “onyo” dhidi yake na wanachama
wengine watano kuwataka wasiendelee na
“mchezo mchafu” wa kampeni za urais
kabla chama hicho hakijaanzisha mchakato
huo rasmi, hapo ndipo wengi wakang’amua
kwamba January anausaka urais wala
hatanii.
Mtoto huyo wa Katibu Mkuu mstaafu wa
CCM, Mzee Yusuph Makamba, aliingia rasmi
kwenye siasa mwaka 2010 alipoomba
ridhaa ya CCM kuwa Mbunge wa Bumbuli,
wilayani Lushoto na katika kura za maoni
za chama hicho, alimshinda mbunge
mzoefu, William Shelukindo kwa kupata
kura 14,612 dhidi ya 1,700. Baada ya
kushinda ndani ya chama chake, January
hakukutana na mpinzani yeyote kwenye
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na hivyo
akaingia kwenye rekodi ya wabunge
waliopita bila kupingwa.
Katika Bunge la 10, alichaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati
na Madini na mwaka 2011, CCM ilimteua
kuwa Katibu wa Idara ya Siasa na
Uhusiano wa Kimataifa akichukua nafasi
ya Benard Membe. Alitumikia wadhifa huo
ndani ya chama chake hadi mwaka 2012
alipomuachia Dk Asha-Rose Migiro.
Katika Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM,
January alichaguliwa kuwa kati ya
wajumbe 10 wa Kamati Kuu ya chama
kutoka upande wa Tanzania Bara akipata
kura 2,093.
Atangaza nia mara ya pili
Juni 7, akiwa Dar es Salaam, January
alitangaza nia kwa mara nyingine ya
kuwania urais akiahidi kwamba Serikali
yake itaunda baraza la mawaziri wasiozidi
18 wasiotiliwa shaka na wananchi juu ya
uwezo na uadilifu wao.
John Pombe Magufuli ni moja kati ya
waliochukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama
cha Mapinduzi ya kupitishwa kugombea nafasi
ya Urais katika uchaguzi mkuu mwezi oktoba
kupitia tiketi ya chama hicho.
Magufuli ni miongoni mwa waliotajwa tano
bora za urais CCM
Dar es Salaam. Kama alivyowashangaza
wengi pale alipojitokeza kuchukua fomu za
kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais
Mei 29 mwaka huu, ndivyo Dk John
Magufuli alivyowashangaza tena jana
kufikia hatua hii ya tano bora.
Bila makeke, majivuno wala majigambo,
Magufuli ambaye ni waziri wa ujenzi
alipochukua fomu alisema tu kuwa
kipaumbelea chake ni kutekeleza ilani ya
uchagzi ya CCM.
Hata katika safari yake ya kusaka
wadhamini mikoani, mbunge huyo wa
Chato alikwenda kimya kimya, bila
mbwembwe, ahadi wala kukusanya
mashabiki.
Bila hiyo ndiyo siri yake ya ushindi,
alihofia kukatwa mapema kwa kukiuka
masharti ya chama, kama ilivyowatokea
wengine.
Hata kabla hajachukua fomu, Dk Magufuli
hakuwahi kutangaza nia yake ya kuwania
urais, hadi alipoibuka ghafla na papo hapo
akapenya hadi hatua hii muhimu, hadi
alipolidokeza gazeti hili mjini Dodoma.
“Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara
zote nimekataa kulijibu kwa sababu katika
chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake
wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi.
Muda ulikuwa haujawadia.
“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa
Dodoma, vikao vya juu vya chama chetu
vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania
nafasi mbalimbali kujitokeza. Kwa maana
hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa
kusema rasmi ‘nitagombea urais’.
“Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo
sifa za kuchagua na kuchaguliwa kama
mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote
inayojitokeza kulingana na Katiba ya chama
chetu na pia Katiba ya nchi,” alisema Dk
Magufuli.
Pamoja na kutokuwa na papara za
kutangaza nia wala kuanza kupitapita kwa
wanachama kutafuta kuungwa mkono, Dk
Magufuli alikuwa vinywani mwa watu
wengi, ndani na nje ya CCM, wakisema
akiteuliwa anaweza kuleta ushindani dhidi
ya upinzani.
Waziri huyo wa muda mrefu na maarufu
kwa kumbukumbu na kukariri takwimu
mbalimbali, kila wizara anayokwenda
inageuka maarufu na kuanza kusikika,
lakini kazi kubwa inayomweka kwenye
mwanga wa kisiasa nap engine hata
kumfikisha katika hatua hii ni wizara ya
Ujenzi na hasa usimamizi wa ujenzi wa
miundombinu.
Dk Magufuli alizaliwa katika Kijiji cha
Rubambangwe kilichopo Wilaya ya Chato
mkoani Geita, ndipo unapoweza kukutana
na wananchi ambao wanafahamu maisha
yake ya ujana na hatua alizopita hadi hadi
hatua ya leo.
Kuna simulizi za kusisimua kuhusu maisha
ya Magufuli ambaye wananchi wengi wa
jimbo lake wanamtumia kama alama ya
ushindi, akihusishwa na mafanikio ya
kujitenga kutoka Wilaya ya Biharamulo
hadi wakapata jimbo na hatimaye Wilaya.
Balozi Amina Salum Ali ni moja kati ya
waliochukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama
cha Mapinduzi ya kupitishwa kugombea nafasi
ya Urais katika uchaguzi mkuu mwezi oktoba
kupitia tiketi ya chama hicho.
Amina Salum Ali ni miongoni mwa waliotajwa
tano bora za urais CCM
Mwanadiplomasia Amina Salum Ali
alitangaza nia ya kuwania urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mei 21
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu nia yake hiyo, Balozi
Amina ambaye alikuwa Balozi wa Kudumu
wa Umoja wa Afrika (AU) kwenye Umoja
wa Mataifa (UN) alisema wanawake
wamekuwa wanyonge kugombea nafasi za
juu za uongozi kwa kukosa fedha, lakini
sasa ni wakati mwafaka kwao kujiamini
katika jamii wakiamini uongozi siyo fedha,
bali ni uzalendo, kujikubali na kujiamini.
“Nimeona nina uzalendo, ninajiamini na
ninaweza kuifikisha nchi yangu katika
uchumi mkubwa kwa kutumia rasilimali
zilizopo, zikiwamo gesi, mafuta, kilimo na
utalii. Ninajiamini kwamba wakati wangu
umefika kuwaongoza Watanzania kwa
kushika nafasi za juu,”alisema.
Balozi Amina ambaye aliwahi kushika
nafasi za juu za uongozi Serikali ya
Zanzibar na ile ya Muungano, ukiwamo
uwaziri wa fedha, alisema Serikali
inatambua mchango wa wanawake katika
jamii, hivyo kupewa nafasi kubwa kama
vile ujaji na uhakimu ni kusaidia kuongeza
ufanisi wao kiutendaji.
“Wanawake wengi wanaogopa kujitokeza
wakihofia kugombea nafasi za juu za
uongozi kwamba kunahitaji fedha, hivyo
wanaishia kuwa wanyonge. Siyo kweli,
wajitokeze kwa wingi ili watimize ndoto za
kuwajibika kwa Taifa lao,” alisema.
Alisema sheria hazitoshelezi kumlinda
mwanamke, lakini mfumo dume
umepungua kwa kiasi kikubwa hata kama
haijafikia asilimia 50 kwa 50, jambo
analosema lazima liangaliwe kwa mtazamo
mpya.
Elimu yake
Balozi Amina alihitimu Chuo Kikuu cha
New Delhi , India - Shahada ya Uchumi
(B.A), mwaka 1979, pia alisomea masuala
ya utawala wa fedha na utafiti wa
uendeshaji kwenye Taasisi ya Uongozi
(Institute of Management) Pune, India
mwaka 1980, pia mwaka 1981 alihitimu
Chuo Kikuu cha Pune, India - (Symbiosis
College of Management) -MBA in Marketing
(Masoko) na mwaka 1983 Chuo Kikuu cha
Helsinki, Finland - Diploma ya utafiti wa
masoko na uuzaji wa bidhaa nje (mafunzo
maalum ya PRODEC).
Nyadhifa alizoshika
Mwaka 1981 hadi 1982, Mchumi
Mwandamizi -Tume ya Mipango Zanzibar,
mwaka 1982 hadi 1983, Mkurugenzi
Biashara za Nje - Wizara ya Biashara ya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mwaka
1983 hadi 984, Katibu Bodi ya Biashara
Zanzibar- Wizara ya Biashara Zanzibar.
Nafasi nyingine ni, mwaka 1984 hadi 1985,
Mchumi Mwandamizi - Tume ya Mipango,
Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar,
mwaka 1985 hadi 1990- Mbunge Bunge la
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, mwaka
1985 hadi 1986- Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, mwaka 1986 hadi 1989-
Waziri wa Nchi ,Wizara ya Mambo ya Nje.
No comments
Post a Comment