Header Ads

Header ADS

Serikali yachunguza ufisadi wa dola mil 6

SERIKALI inachunguza ufisadi wa Dola za Marekani milioni sita, ambazo Benki ya Stanbic Tanzania pamoja na Kampuni ya Egma ya nchini, iliongeza katika malipo ya ada ya mkopo, ambao Serikali iliomba kwa Benki ya Standard ya Uingereza mwaka 2013.
Imesema inafanya uchunguzi wa ndani ili kubaini fedha hizo za kigeni zilizoingizwa kwenye akaunti ya Egma, zimekwenda wapi na kama zilitumika kuhonga, zimemhonga nani. Akizungumza na waandishi wa habari jana Ikulu Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hatua hiyo imekuja baada ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO) kushinda kesi katika Mahakama ya Southwark Crown ya Uingereza dhidi ya Stanbic Tanzania inayomilikiwa na Standard Group.
“Sasa baada ya Taasisi ya SFO kushinda kesi, Tanzania tunarudi kufanya uchunguzi wa ndani kubaini hizo fedha dola milioni sita zilizoingizwa kwenye akaunti ya kampuni ya Egma na kutolewa zote muda mfupi zimekwenda wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu, ni nani,” alifafanua Balozi Sefue.
Balozi Sefue aliwataja wamiliki wa Egma kuwa ni aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Mitaji Tanzania, Fratern Mboya na Mkurugenzi Gasper Njuu.
Alitoa mwito kwa wamiliki hao, kutoa ushirikiano wakati wa uchunguzi wa sakata hilo na kwamba mara baada ya uchunguzi kukamilika, iwapo kutabainika makosa ya rushwa au mengine, sheria itachukua mkondo wake.
“Ombi letu na ombi la Rais John Magufuli watu hawa wanatakiwa kutoa ushirikiano na pengine ameongezeka mmiliki kwenye kampuni hiyo, wahakikishe wanatoa ushirikiano,” alisisitiza Balozi Sefue. Akizungumzia sakata hilo, Balozi Sefue alisema sio jambo geni kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari nchini vimeripoti jana, na kwamba tangu mwaka 2013, Tanzania inalifahamu na ndiyo iliyolipeleka SFO kuchunguzwa.
Akifafanua, alisema katika mwaka 2012/13, serikali ilifanya utaratibu wa kawaida unaofanywa na nchi mbalimbali duniani wa kukopa kwenye taasisi za benki ambapo Benki ya Standard ilikubali kuikopesha.
Alisema katika mkopo huo, serikali ilihitaji Dola za Marekani milioni 600 kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo kwa kawaida benki husika huingia mkataba na benki nyingine inayopewa jukumu la kutoa mkopo huo.
Alisema katika mchakato huo, Benki ya Standard kupitia kampuni tanzu iliipa Benki ya Stanbic Tanzania kazi hiyo ambapo fedha hizo zilipatikana na kwamba katika mchakato wa mkopo huo, ada ya mkopo serikali ilitozwa asilimia 2.4 ya mkopo.
Aliyataja masharti mengine kwamba yalikuwa ni kulipa mkopo riba kwa miaka saba, na kwamba deni hilo litalipwa kwa miaka saba, ambapo linapaswa kumalizika mwaka 2019. Balozi Sefue alifafanua kwamba baada ya mkopo kutolewa nusu ya kwanza, Mtendaji Mkuu wa benki hiyo wakati huo, Bashir Awale alikuwa na matatizo na watumishi, na Benki Kuu (BoT) iliingilia kati na kufanya uchunguzi.
Katika uchunguzi huo, kulibainika kasoro nyingi zikiwemo ulipaji wa fedha kwenye kampuni bila maelezo ikiwemo Kampuni ya Egma ambayo ilibainika kulipwa Dola za Marekani milioni sita.
Alisema fedha hizo zilionekana zimeingizwa kwenye Egma na kutolewa zote bila kutozwa kodi, ambapo katika taarifa yao ya ukaguzi, BoT ililionesha hilo na mambo mengine yaliyobaini na kumkabidhi Mwenyekiti wa Benki ya Stanbic Tanzania.
Hata hivyo, baada ya taarifa hiyo kupokewa, mwenyekiti wa benki hiyo aliitisha mkutano wa Bodi ya benki na waliipitia taarifa hiyo ya BoT na taarifa kupeleka Kitengo ya Uchunguzi cha Kimataifa cha Intelijensia.
Alisema katika uchunguzi huo, ndipo ilibainika kwamba nchi ilitozwa ada zaidi, ambapo ada ya mkopo halali ilikuwa Dola za Marekani milioni 1.4, lakini Stanbic walichukua Dola za Marekani milioni 2.4.
Alisema fedha hizo zilizoamriwa na Mahakama nchini Uingereza kwamba Benki ya Standard iilipe Tanzania ni zile ambazo hazikupaswa kuchukuliwa, ambazo ni dola milioni sita na dola milioni moja ni faida.

No comments

Powered by Blogger.