Vyama vitakavyoshiriki uchaguzi marudio Zanzibar
VYAMA vitano vya siasa vitashiriki katika uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, utakaofanyika Machi 20 mwaka huu, uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ADC, CCK, TLP na SAU.
Hatua hiyo inatokana na vyama vitatu vya siasa Zanzibar vya CCK, SAU na TLP, kutangaza kuwa wagombea wake, watashiriki katika uchaguzi huo wa Machi 20. Taarifa ya viongozi wa vyama vya CCK, SAU na TLP, iliyosomwa kwa pamoja katika Ukumbi wa Culture eneo la Mji Mkongwe mjini hapa jana, ilisema wagombea wa vyama hivyo vitatu, watashiriki uchaguzi huo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ulifutwa baada ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali, zilizoonesha wazi kwamba hauwezi tena kuwa huru na haki. Wagombea wa vyama hivyo vya siasa, waliotangaza kushiriki katika uchaguzi huo ni Ali Khatib kutoka CCK, Issa Mohamed Zonga kutoka SAU na Hafidh Hassan Simai kutoka TLP.
Mgombea wa CCK, Ali Khatib Ali alisema kwamba tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi huo na kuwataka wanachama na wafuasi wake na wananchi, kuitumia fursa hiyo ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaoongoza nchi. “Tangazo la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) limetutaka kurudia uchaguzi kwa sababu ule wa awali umefutwa kwa hivyo hatuna sababu ya kususia uchaguzi huo na tunachofanya kwa sasa ni kuwataka wanachama wetu na wafuasi kujitayarisha kwa uchaguzi wa marudio,” alisema Ali.
Jumapili iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema chama hicho kipo tayari kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 kwa lengo la kuhakikisha kinashika dola. Akihutubia mamia ya wanachama wao katika viwanja vya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui wakati wa kuzindua maadhimisho ya miaka 39 ya CCM, Dk Shein alisema maamuzi ya kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu, yamefanywa na ZEC ambayo ndiyo chombo halali kwa mujibu wa Katiba cha kushughulikia masuala yote ya uchaguzi nchini.
Aliwataka wanachama na wafuasi wao kujipanga vizuri na kushiriki uchaguzi huo kikamilifu, kwani kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni kushinda chaguzi zote zinazofanyika nchini ili kushika dola na kuwatumikia wananchi. “Hayo ndiyo maamuzi ya chama chetu tuliyokubaliana kushiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio baada ya kufutwa kwa ule wa Oktoba 25 mwaka jana kwa hivyo wanachama na wafuasi jitayarisheni kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kushika dola,” alisema Dk Shein.
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam limevisihi vyama vya siasa vya Zanzibar kikiwemo Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kimetangaza kususia uchaguzi wa marudio, kushiriki uchaguzi huo kwa maslahi ya Taifa. Aidha, limeitaka ZEC kuhakikisha inasimamia uchaguzi huo kwa haki, uadilifu na umakini mkubwa huku wakimuogopa Mungu na kutambua kuwa kama hawatatenda haki, wataulizwa katika siku za mwisho.
Hayo yalielezwa na Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana. Alieleza kuwa Baraza hilo, haliwezi kukaa kimya kana kwamba suala la Zanzibar haliwahusu Watanzania Bara, bali linawahusu Watanzania wote kwa kuwa ni ndugu wa damu. “Sisi Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam tunaunga mkono hatua ya ZEC kufanya uchaguzi wa marudio...vile vile tunakiomba chama cha CUF ambacho kimetangaza kususia uchaguzi huo na vyama vingine vyote, viache kususia bali vijipange kwa ajili ya kushiriki.
“Lakini pia tunawaomba ZEC kulisimamia zoezi hilo kwa haki na umakini mkubwa kwa maslahi ya taifa... pia wamuogope Mungu wakumbuke hii dunia tunapita, wasipotenda haki wataulizwa na Mwenyezi Mungu kwanini walisimamia batili,” alisema Shehe Salum. Aidha, alisema barua aliyoipokea kutoka kwa Amir wa Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmad ambaye yuko gerezani, imeeleza kuwa anaunga mkono suala la kufanya uchaguzi wa marudio kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kumaliza mgogoro huo, na kuwa hakuna njia mbadala.
Alisema katika barua hiyo, Shehe Farid aligusia mambo matatu ambapo hata hivyo mambo mengine mawili ambayo yameandikwa katika barua hiyo, hakuyataja yalizungumzia nini. Aliwataka Wazanzibari kuhakikisha wanadumisha amani na utulivu walionao na kulinda umoja na mshikamano, kwani amani itakapovurugika, haitaishia Zanzibar pekee, bali itagusa hadi Bara hivyo wanatakiwa kuwa watulivu.
Aidha, Bakwata imepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli kutokana na hatua mbalimbali inazozichukua, zenye lengo la kuimarisha nidhamu, hasa kwa watumishi wa umma na serikali. Shehe Salum alisema hatua hizo, zimeanza kuleta tija kubwa kwa taifa kwani hata pato la serikali limekuwa likiongezeka mwezi hadi mwezi.
Aidha, baraza hilo limeiomba serikali kuendelea kutatua changamoto mbalimbali hasa zilizoko ndani ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwemo kulipa umuhimu unaostahili Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kwani suala la foleni linachangia kuzorotesha uchumi wa Taifa kutokana na kuwa wafanyakazi wengi wanategemea usafiri wa daladala.
“Aidha, tunapongeza dhamira yake ya kubana matumizi ya serikali na badala yake kuelekeza fedha kwenye huduma za jamii na tayari tumeshaanza kunufaika na huduma hizo,” alisema. Alisema huduma hizo ni pamoja na elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, kwani linalopaswa kupongezwa kwa kuwa ada za shule na gharama za kuandikisha watoto zilikuwa ni mzigo kwa wananchi wengi.
“Ni muhimu Serikali kuwasaidia wawekezaji wa ndani kama hawa Simon Group, wamefanya kazi nzuri na kama kuna masharti magumu wamewekewa serikali ione namna ya kuwasaidia kwa kuwa wananchi wanahitaji usafiri huo wa mabasi ya mwendo kasi ili waondokane na adha ya foleni, walete ufanisi katika kazi zao.
Ndivyo wanavyofanya duniani kote wawekezaji wa ndani wanasaidiwa,” alisema Shehe wa Mkoa. Imeandikwa na Katuma Masamba, Dar na Khatib Suleiman, Zanzibar
No comments
Post a Comment