Header Ads

Header ADS

Wanafunzi 96,018 wachaguliwa kidato cha tano

WANAFUNZI 96,018 sawa na asilimia 27.60 ya waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka jana, na kupata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu, wamechaguliwa kujiunga na masomo ya Kidato cha Tano na vyuo vya ufundi vya serikali kuanzia mwezi ujao.
Aidha, ufaulu katika mwaka 2016 uliongezeka kwa asilimia 3.15 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2015. Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, asilimia 27.60 imevuka lengo lililowekwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayoielekeza serikali kuhakikisha asilimia 20 ya wanafunzi wa elimumsingi wanachaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano.
Akitangaza uchaguzi na upangaji wa wanafunzi hao wa kujiunga na Kidato cha Tano jana ofisini kwake mjini hapa, Simbachawene alisema jumla ya watahiniwa wa shule 349,524 wakiwamo wasichana 178,775 (51.1%) na wavulana 170,749 (48.9%) walifanya mtihani wa kumaliza Kidato cha Nne mwaka 2016.
“Watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo mwaka 2016 walikuwa 47,751 wakiwemo wasichana 24,587 sawa na asilimia 51.5 na wavulana 23,164 sawa na asilimia 48.5,” alieleza Simbachawene.
Alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2017 wanatoka kwenye shule za serikali na zisizo za serikali, na shule 351 zikiwamo shule 17 mpya zimepangiwa wanafunzi hao 96,018.
“Kati ya wanafunzi 96,018 ni wa wanafunzi 93,019 ndio wenye sifa za kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo Vya Ufundi kwa kuwa wamefaulu vigezo vyote vya msingi kama vilivyoanishwa,” alifafanua.
Aliongeza kuwa kati ya hao, wanafunzi 92,998 ni wa shule na wanafunzi 21 walisoma chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW). Alivitaja vigezo vilivyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia vilivyotumika kuchagua na kupanga wanafunzi wa Kidato cha Tano kuwa ni AAA hadi CCD kama cut off point kwenye masomo ya tahasusi, alama tatu (credit) na pointi zisizopungua 25 kwenye Daraja, machaguo yaliyojazwa na mwanafunzi kwenye fomu maalumu na nafasi zilizopo katika shule husika.
“Napenda kusisitiza kwamba vigezo hivi ndivyo vinavyotumika kwa mwanafunzi kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo Vya Ufundi kwa mwaka huu. Nia ni kuinua kiwango cha elimu na ujuzi kwa elimu ya juu nchini,” alifafanua Simbachawene.
Kuhusu tarehe ya kuripoti shuleni, alisema muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano mwaka 2017, utaanza Julai 17, mwaka huu, lakini kwa wanafunzi wanaoingia Kidato cha Sita watafungua shule Julai 3.
“Kwa kuwa upangaji wa wanafunzi wanaoingia Kiato cha Tano kwa mwaka 2017 umezingatia machaguo ya wanafunzi wenyewe na nafasi zilizopo katika shule husika, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule,” alieleza Waziri wa Tamisemi.
Aliwaagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati, na endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya kufungua shule, nafasi yake itachukuliwa na wanafunzi wengine.
Aidha, aliwaelekeza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kuhakikisha kuwa shule zililizopelekewa fedha za kuongeza miundombinu ya Kidato cha Tano kupitia Mpango wa Elimu Lipa kulingana na Matokeo (EP4R) zinakamilisha ujenzi kabla ya Juni 30, 2017, na kuwapokea wanafunzi wa Kidato cha Tano.
“Napenda kuwapongeza walimu wote kwa juhudi walizozifanya katika ufundishaji na kuwezesha wanafunzi kufaulu vizuri. Hii imetokana na ushirikiano wa walimu, wazazi na walezi katika kuwapatia wanafunzi hao malezi bora,” aliongeza waziri.
Aliwapongeza wanafunzi waliochaguliwa, akiwahimiza kuendelea kuongeza bidii katika kujifunza ili wafanikiwe kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu baada ya kuhitimu Kidato cha Sita.
Aidha, aliwashukuru wadau wa elimu kwa maana ya viongozi na watendaji wa mikoa, wilaya na halmashauri pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kushiriki kikamilifu kuimarisha miundombinu ya shule, ikiwemo maabara na majengo mengine muhimu, yaliyowezesha shule kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano kwa mara ya kwanza.

No comments

Powered by Blogger.