SIKU 15 alizotoa Rais John Magufuli kwa wakuu wa mikoa, wawe
wamejumlisha wafanyakazi wote na kuhakikisha wanaondoa wafanyakazi hewa,
zimetimia leo. Baadhi ya mikoa imeanika idadi ya watumishi hewa,
waliobainika kupitia uhakiki huo, lakini mingi haijafanya hivyo.
Agizo hilo la Rais Magufuli ni sehemu ya maagizo kadhaa aliyotoa
Machi 15 mwaka huu wakati akiwaapisha wakuu hao wa mikoa jijini Dar es
Salaam; ambao aliwasisitiza kuwa ili mradi wamekubali kushika wadhifa
huo, wameingia kwenye mtego.
Pamoja na majukumu mengine waliyopewa kuhakikisha wanayatekeleza
katika uongozi wao, suala la watumishi hewa ni mtego unaowakabili wakuu
hao wa mikoa wakipaswa kujinasua nao ndani ya wiki hii ambao siku
zilizotolewa zimefika ukomo; Vinginevyo, wataweka rehani nyadhifa zao.
Majukumu mengine ambayo wakuu hao wa mikoa walipewa na Rais
wahakikishe wanayatekeleza, ni pamoja na kukabili ujambazi hususan wakuu
wa mikoa ya pembezoni inayokabiliwa na tatizo la utekaji magari kiasi
cha serikali kuamua kuweka utaratibu wa polisi kuyasindikiza.
Mengine ni kukabili watu wazembe, watendaji wanaowanyanyasa wananchi,
njaa, kodi za mazao, migogoro ya ardhi na kuhakikisha wanasimamia
mpango wa elimu bure unafanikiwa.
Tangu Rais atoe maelekezo hayo ya kukabili wafanyakazi hewa, mikoa
mbalimbali inaendelea na mchakato wa kuhakiki wafanyakazi kwenye idara
na taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwataka watumishi kuwasilisha
nyaraka mbalimbali ikiwemo barua za ajira.
Katika mchakato huo ambao umezaa matunda kwa kubaini watumishi hewa
waliokuwa wakilipwa mishahara, baadhi ya halmashauri zililazimika kufuta
huku baadhi ya halmashauri zimeamuru watumishi wake walio masomoni na
kwenye likizo, warudi mara moja katika vituo vyao vya kazi kuhakikiwa.
Madudu yaibuliwa Miongoni mwa mikoa ambayo imetoa taarifa za uhakiki
ni pamoja na mkoa wa Dodoma, ambao umetajwa kuwa na watumishi hewa 144.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, ameagiza kupelekewa orodha ya
watumishi hao na wakati huo huo kupatiwa maelezo kwa nini kuna watumishi
hewa na kutaka kupatiwa orodha za watumishi hao.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa makabidhiano ya ofisi na
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa aliyehamia Mkoa wa
Songwe, Rugimbana alisema uhakiki wa watumishi wa serikali umebaini
uwepo wa idadi hiyo ya watumishi hewa .
Mkoa wa Kigoma pia ni miongoni mwa mikoa ambayo taarifa zake za
uhakiki zimeshatolewa ambako imebainika kuwapo watumishi hewa 169 kwa
kipindi cha mwaka uliopita.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emanuel Maganga amewataka wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi wote waliopo katika halmashauri zote kutaja kiasi
cha fedha kilichotumika kulipa mishahara watumishi hewa hao 169 ndani
ya kipindi hicho cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo wa Kigoma, watumishi hewa
waliowabaini, wamo waliokwishafukuzwa, waliofariki na wengine wasiokuwa
na sifa za kuwa watumishi wa umma.
Maganga ametaka fedha walizokuwa wakilipwa watumishi hao hewa kwa
ajili ya mishahara, zirudi na wakati huo huo wakurugenzi wawafute kwenye
orodha ya malipo.
Halmashauri za mkoa wa Kigoma zenye watumishi hewa na idadi yake
kwenye mabano ni Kasulu (78), Kigoma (23), Manispaa ya Kigoma Ujiji
(29), Buhigwe (11), Uvinza (19), Kibondo (5) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
yenye watumishi hewa wanne.
Halmashauri ya Kakonko ndiyo pekee isiyo na mtumishi hewa.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Evarist Ndikilo, alisema leo ambayo ndiyo ukomo wa muda aliotoa Rais,
atatoa taarifa kamili ya kazi hiyo ya kuhakiki wafanyakazi na kuondoa
wafanyakazi hewa watakaokuwa wamebainika.
Ndikilo alisema, ipo timu inayo endelea kufanya uhakiki kwenye wilaya
mbalimbali kwa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri. Likizo
zaahirishwa Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam, Halmashauri ya wilaya
ya Temeke ililazimika kuwaita watumishi wake walioko masomoni na likizo
kurudi mara moja katika vituo vyao vya kazi wahakikiwe.
Msemaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Joyce Nsumba alisema hivi
karibuni uhakiki uliendelea kwa makundi mbalimbali wakiwemo watumishi
kutoka Idara ya Afya, Elimu, Fedha na Biashara, Kilimo, Mifugo, Ujenzi
na Maendeleo ya Jamii.
Wakati anazungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Nsumba
alisema walishahakiki watumishi 8,000. Sababu za uhakiki Uamuzi wa Rais
Magufuli kuamuru ufanyike uhakiki, ulitokana na uchunguzi uliofanywa
katika mikoa ya Singida na Dodoma katika halmashauri 14 na kugundulika
kwa watumishi hewa 202 wanaolipwa mishahara.
Aliagiza uhakiki kwa watumishi wote katika wizara, mikoa, wilaya,
idara,taasisi na Wakala za Serikali ndani ya siku 15. “Sasa niwaombe
ndugu zangu wakuu wa mikoa, najua mtakwenda kuwapa maagizo wakurugenzi
na wakuu wa wilaya.
Lakini niwape muda, ndani ya siku 15, wawe wamejumlisha wafanyakazi
wote, wamewatoa wafanyakazi hewa,” ali waagiza. Rais Magufuli alisema
mshahara ujao, ikigundulika kuwapo wafanyakazi hewa kwenye orodha ya
malipo, mkurugenzi husika ajihesabu hana kazi na atafikishwa mahakamani.
Vile vile amewaambia mawaziri, hususan Waziri wa Fedha na Mipango
aliyekuwapo kwenye hafla hiyo, wakawaeleze watendaji kwenye wizara zao
na taasisi mbalimbali wahakikishe wanawaondoa wafanyakazi hewa ndani ya
siku 15 na wasipotimiza agizo hilo hatua zitakuwa ni zilezile kwani
sheria ni msumeno.
Alisema inasikitisha kuona fedha zinazokusanywa haziendi kwenye
miradi inayopangwa, badala yake sehemu kubwa inatumika kulipa mishahara
ikiwemo hewa. Alisema kwa ujumla Serikali inalipa mishahara kila mwezi
kwa watumishi wake wa umma jumla ya Sh bilioni 549 mpaka bilioni 550.
Alisema kwa hali ilivyo, fedha nyingi zinaishia kwenye mishahara
feki. Nawapa Ma-RC siku 15 mhakikishe Wakurugenzi wa halmashauri zote
wamejumlisha idadi ya wafanyakazi wote waliopo na kuondoa wafanyakazi
hewa katika halmashauri zao,” alisisitiza Rais Magufuli.
Mikoa ya Tanzania Bara ni: Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga,
Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi,
Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida, Tabora,
Pwani, Manyara, Mara, Morogoro na Kilimanjaro