WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako amesitisha ajira ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), George Nyatega kwa tuhuma za udhaifu
katika fedha za mikopo zaidi ya Sh bilioni 3.2.
Pia amewasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa Fedha na Utawala,
Urejeshaji Mikopo na Upangaji na Utoaji Mikopo katika HESLB kwa tuhuma
za udhaifu huo wa mikopo ya Sh 3,234,452,259.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa
Ndalichako alisema hatua hiyo, imechukuliwa baada ya kuridhika na kuona
utendaji usioridhisha kwenye taasisi hiyo, kiasi cha kuwapo matatizo
mengi yanayojirudiarudia kwa wateja wao, ikiwamo ucheleweshaji wa mikopo
bila sababu ya msingi.
Profesa Ndalichako alisema pia uongozi wa bodi hiyo, umeshindwa kutoa
majibu ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, alipoagizwa na Wizara
Januari mwaka huu.
“Majibu yaliyowasilishwa na Bodi Februari 1, mwaka huu yanadai kuwa
taarifa ya mkaguzi haikukidhi viwango na kwamba ilijikita katika
‘operational audit’, wakati kazi hiyo hufanywa na mkaguzi wao wa ndani.
Pia walikiri baadhi ya udhaifu kama kusajili mara mbili ambao ulitokana
na kuwa wakati huo walikuwa hawajaanza kutumia mfumo wa kompyuta,”
alieleza Waziri wa Elimu.
Aliongeza: “Kwa mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa Kifungu D.5(3) cha
Kanuni za Kudumu kinachohusu uteuzi wa maofisa wa juu wa taasisi za
serikali na Kifungu D.12 kinachoruhusu utoaji wa taarifa za Mtendaji na
Kifungu F.50(1) kinachohusu usitishaji wa mkataba na kile cha Bodi ya
Mikopo Kifungu cha 11(3), nimesitisha mkataba wa ajira wa George
Nyatega,” alieleza Profesa Ndalichako.
Alisema kutokana na kusitisha ajira ya kiongozi huyo, Bodi inatakiwa
kumlipa mshahara wa mwezi mmoja kama notisi kulingana na Kifungu
50(3)(a) cha Kanuni za Kudumu. Nyatega alikuwa astaafu Agosti 31, mwaka
huu baada ya kuwa aliongezewa mkataba wa miaka miwili baada ya kustaafu
Machi 2014, na kuongezewa mkataba kuanzia Septemba 2014.
Alisema pia amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha na Utawala,
Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo Juma Chagonja na
Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer na kuwa wizara
itateua maofisa watakaoshika nafasi hizo hadi uchunguzi utakapokamilika
na wakurugenzi hao kuchukuliwa hatua stahiki.
“Namwagiza Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ahakiki maelezo na
nyaraka zilizowasilishwa na Bodi ya Mikopo pamoja na kufanya ukaguzi
maalumu kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi sasa ukaguzi uanze mara
moja,” alieleza Profesa Ndalichako.
Akifafanua zaidi kuhusu malipo yasiyo sahihi, alisema: “baadhi ya
wanafunzi ambao walikwenda kusoma Algeria wamekuwa wakiendelea kulipwa
fedha wakati mkataba wao wa mkopo wa miaka minne umekwisha, lakini
wamelipwa hadi miaka saba kinyume cha utaratibu.”
Alisema ukaguzi huo wa mwaka 2013, umebainisha kuwa wanafunzi 23
walipata mikopo kupitia vyuo viwili tofauti na walilipwa jumla ya Sh
153,999,590 katika chuo kimoja na Sh 147,541,460 katika chuo cha pili
ambazo zimelipwa miaka mitatu mfululizo.
Waziri alisema pia wanafunzi 169 walilipwa mikopo kupitia vyuo viwili
tofauti ambapo Sh 658,047,570 zililipwa katika chuo cha kwanza na Sh
665,135,716 chuo cha pili zilizolipwa kwa miaka miwili mfululizo.
Alisema pia wanafunzi 343 wasiokuwa na usajili kwenye vyuo husika
walilipwa Sh 342,468,500 huku wanafunzi 55 walioacha masomo walilipwa Sh
136,232,800.
“Jumla ya Sh 159,664,500 zililipwa kwa wanafunzi 306 zaidi ya kiwango
kilichobainishwa kwenye vipengele namba 4.3 na 4.3.2 cha miongozo ya
upangaji na ukopaji ya mwaka 2008/2009 na 2009/2010 na vipengele no 4.6
na 4.3.1 cha miongozo ya upangaji na ukopeshaji mikopo ya mwaka
2008.2009 na 2009/2010 hadi 2010/2011."
Alifafanua kuwa pia wanafunzi 77 walipatiwa mikopo kwenye vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja.
Wanafunzi hao walitumiwa Sh 467,620,654 kwa vyuo vya nje na Sh
123,047,119 ya vyuo vya ndani huku wanafunzi 19,348 walipatiwa mikopo
bila kupitishwa na Kamati ya Mikopo wakati wanafunzi 54,299 walipangiwa
mikopo wakati hawakuwa wameomba.
Alisema kuwa pia Bodi ilipeleka Sh 207,052,650 kwenye vituo sita vya
elimu ya juu na kutochukuliwa na wanafunzi husika na fedha hizo
hazikurejeshwa Bodi kinyume cha Hati ya Makubaliano (MOU) kifungu
3.3.4(b) na (c).
“Ukaguzi utakwenda mpaka kwenye vyuo, endapo tutabaini vyuo kiwe cha
umma au binafsi wamehusika kushirikiana na watendaji wa Bodi kuhujumu
fedha tutachukua hatua za kisheria dhidi yao. “Nazionya taasisi zilizo
chini ya wizara, sitakuwa tayari kuona wanafunzi wanakaa chini, hawana
madarasa halafu kuna taasisi zinahujumu hata senti tano, tutaendelea
kuzifuatilia kwa karibu,” alionya Profesa Ndalichako.
Katika hatua nyingine, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA)
limekanusha taarifa zilizosambazwa jana katika mitandao ya kijamii kuwa
limezuia matokeo hadi yasahihishwe upya, kuwa si za kweli na kwamba
mchakato wa kutunuku uko katika hatua nzuri; kwa mujibu wa Ofisa Habari
wa Necta, John Nchimbi.