Madam Ritha akiwatambulisha washiriki.
SHINDANO
la kusaka vipaji vya muziki, Bongo Star Search (BSS) linalotarajiwa
kufanyika Oktoba 9, limeongeza zawadi ya mshindi wa shindano hilo
ambapo sasa atajinyakulia shilingi milioni 60, ambapo shilingi milioni
kumi zitapelekwa studio kwa ajili ya kusaidia shughuli za kurekodi.
Akizungumza
mbele ya waandishi wa habari, Jaji Mkuu wa shindano hilo Ritha Paulsen
‘Madam Ritha’, alisema kuwa shindano hilo lina msisimuko wa kipekee
kwa kuwa washiriki wote ni wazuri kiasi majaji wanapata wakati mgumu
kumchagua mshindi.
“Mshindi
wa shindano hili ataondoka na sh. milioni 60, katika kinyang’anyiro cha
safari hii chenye msisimko mkubwa hadi hata sisi wenyewe tunapata
wakati mgumu kama majaji,” alisema Ritha
Fainali
za shindano hilo zinatarajiwa kufanyika Ijumaa Oktoba 9 Mwaka huu
katika Ukumbi wa King Solomon uliopo eneo la Namanga Kinondoni jijini
Dar es Salaam. Siku hiyo pia kutakuwa na burudani za nguvu kutoka kwa
msanii Run Town wa Nigeria ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wake wa
Gallardo.
“Ukiachia
mbali msanii huyo pia kutakuwa na burudani kutoka kwa Christian Bella,
Yamoto Bendi, Nevy Kenzo ambao watakamua sambamba na wasanii mahiri
ambao ni zao la BSS kama Peter Msechu na Kala Jeremiah. Viingilio siku
hiyo vitakuwa 25,000/=, ambapo nafasi za VIP zitakuwa 50,000/= na viti
maalum vitalipiwa 100,000/=. Nawaomba mashabiki waje kwa wingi maana
fainali ya mwaka huu ni ya kipekee kabisa,” alisema Madam Ritha.
|
No comments
Post a Comment