maelfu wajitokeza kumuaga Mchungaji Mtikila
RAIS Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji pamoja na viongozi wa kitaifa, katika kumuaga Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila aliyekufa kwa ajali hivi karibuni mkoani Pwani.
Katika shughuli hiyo, viongozi wengi waliohudhuria walimuelezea Mtikila kuwa ni mwanaharakati wa mageuzi, aliyeipigania Tanganyika mpaka kifo chake, lakini pia alisimamia na kuheshimu taratibu za kisheria na kutaka mabadiliko bila uoga.
Rais Kikwete alifika katika shughuli hiyo ya kumuaga Mtikila iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, akiambatana na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Viongozi wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Msajili wa zamani wa vyama hivyo, John Tendwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.
Pia walikuwepo Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Mziray ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha PPT-Maendeleo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari na Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Dotnata Rwechungura.
Akizungumza katika shughuli hiyo ya kumuaga Mtikila ambaye jeneza lake lilifunikwa kwa bendera ya Tanganyika, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mutungi aliwataka watanzania kumuenzi mchungaji huyo kwa matendo yake ya kuchukia vurugu na badala yake aliamini zaidi katika sheria.
“Mchungaji Mtikila atakumbukwa kwa misimamo yake mikali. Alipenda kusimamia kile anachokiamini. Lakini kubwa zaidi alitoa mchango katika nyanja ya Sheria, kwa sasa huwezi kuzungumzia masuala ya sheria hususani haki za binadamu bila kumtaja Mtikila,” alisema Mutungi.
Alisema kupitia sekta ya Sheria, mwanaharakati huyo alifanikisha mabadiliko kadhaa, ikiwemo kuingizwa kwenye Katiba kwa kifungu kinachoruhusu mgombea binafsi, lakini pia alifanikisha kubadilishwa kwa kifungu kinachohusu maandamano.
“Huyu alikuwa ni mpambanaji, alifungua kesi nyingi kwa kuwa aliamini katika kufuata sheria na si kuandamana au kufanya vurugu. Naomba tumuenzi kwa kutopenda kushinikiza fujo na maandamano, vyombo vya sheria vipo kama kuna tatizo tuvitumie kutafuta haki,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Dk Bilal alimtaja Mchungaji Mtikila kuwa alikuwa ni mtu jasiri, aliyeshirikiana na wenzake bila kujali tofauti za mitazamo waliyonayo. “Mimi nilimfahamu Mtikila kupitia uanaharakati wake wa kutaka mabadiliko, ni kweli alikuwa anataka sana kuirejesha Tanganyika, lakini pamoja na tofauti za fikra zetu, alikuwa anakuja hadi ofisini kwangu kipindi kile nilikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia na tulikuwa tunazungumza sana,” alisema.
Aliwataka watanzania kuiga mfano wa matendo ya Mtikila, kwani kwa sasa nchi inataka watu kama hao wenye mawazo mapya na hawaogopi kuyatoa na kuyatetea bila kudharau mawazo na fikra za wengine.
Maalim Seif, kwa upande wake, alisema alifahamiana na Mtikila kupitia harakati zake za kisiasa na kubainisha kuwa ni mtu anayejiamini, asiye uoga na mwenye kuajimini na kusimamia kile anachokiamini.
Mziray alisema anaipongeza Serikali kwa kitendo chake cha kushirikiana na familia ya Mtikila kwa hali na mali, bila kujadili kuwa ni mwanaharakati wa mabadiliko, jambo alilosisitiza kuwa hiyo ndio Tanzania inayotakiwa kwa sasa.
Makamu Mwenyekiti wa DP, Peter Mwagila alibainisha kuwa chama hicho kimepata pigo na pengo kubwa kwa kuondokewa na mwenyekiti wao, ambaye pia pamoja na kuwa muasisi wa chama hicho, ni mwanaharakati wa mageuzi aliyepigania nchi yake ya Tanganyika.
“Mtikila ndoto zake zilikuwa ni kurejeshwa kwa Tanganyika ambayo iliondolewa kwenye ramani ya dunia tangu mwaka 1962, alitaka kuwepo na Rais wa Tanganyika, Katiba, wabunge na mamlaka zote za nchi ya Tanganyika. Lakini pia alipinga rushwa, ufisaidi na kuwachukia viongozi wanaojilimbikizia mali,” alisema.
Alisema chama hicho kitahakikisha kinaendeleza na kusimamia harakati zote zilizoanzishwa na Mtikila ikiwemo kuidai Tanganyika. Msemaji wa familia ya mchungaji huyo, Peter Mayani, wakati akisoma wasifu wa Mtikila, alisema mwanaharakati huyo alibobea katika fani za sheria, uchumi na masoko na aliwahi kuajiriwa Mahakama Kuu na Shirika la Ndege la Afrika Mashariki, ambalo alilitumia kutoroshea wanaharakati wa chama cha Frelimo.
Alisema Mtikila aliokoka rasmi mwaka 1983 na kuanzisha Kanisa la Pentekoste la Full Salvation na mwaka 1990 alianza harakati za ukombozi, zilizoshinikiza kuanzishwa kwa vyama vingi mwaka 1992. Pia alianzisha chama cha DP, ambacho kilichelewa kupata usajili wake hadi mwaka 2000.
Mtikila baada ya kuagwa alisafirishwa kwenda kijijini kwao Milo, wilayani Ludewa mkoani Njombe ambako anatarajiwa kuzikwa leo. Marehemu ameacha mjane Georgia Mtikila. Askofu wa Kanisa la Ufunuo, Nabii Paul Bendera, aliwataka watanzania kutambua kuwa wote ni wageni duniani na kwamba kila mtu bila kujali ni nani duniani na ana cheo gani iko siku yake atakufa.
“Kwa sasa hali imekuwa ngumu na mbaya nawaomba ndugu zangu tuwe makini, lakini kubwa zaidi kila mtu amheshimu maisha ya mwenzake tuweke upendo na amani mbele na hii iwe ndio kipaumbele chetu. Naomba Serikali nayo iongeze juhudi za kuwalinda wananchi wake,” alisisitiza.
Mchungaji Daudi Mwaijojele, alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania kuacha uchafu na kumrejea Mungu, ili kutengeneza maisha yao ya baadaye pindi watakapokufa. “Nawaomba acheni uchangudua, ufisadi na michepuko tena hiyo michepuko ndio inaleta magonjwa kama vile Ukimwi majumbwani na kusambaratisha familia,” alisema.
Mtikila alikufa kwa ajali ya gari aina ya Toyota Corolla, lenye namba za usajili T 189 AGM maeneo ya Msolwa wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani. Alikuwa akitokea Njombe kwenda Dar es Salaam.
No comments
Post a Comment