TAARIFA YA CCM KWA VYOMBO VYA HABARI, OKTOBA 28, 2015


TAARIFA YA CCM KWA VYOMBO VYA HABARI, OKTOBA 28, 2015

 
CCM inapenda kutoa taarifa ifuatayo
kwa wana-CCM na kwa umma:
MALALAMIKO YA CCM KUHUSU
MATOKEO KWENYE BAADHI YA
MAJIMBO
Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa
na utaratibu wa kukusanya na
kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya
majimbo. Katika majimbo manne
kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa
utaratibu wa uchaguzi, hasa katika
kujumlisha matokeo, uliopelekea
wabunge wa upinzani kutangazwa
washindi. Majimbo hayo ni Iringa
Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe.
Wasimamizi wa uchaguzi katika
majimbo haya wamevuruga uchaguzi.
Kutokana na utata uliokuwa
umejitokeza wakati wa zoezi la
kujumlisha kura, CCM iliomba kura
zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki
hiyo ya msingi ambayo iko kwenye
sheria. Kwenye baadhi ya majimbo,
ikiwemo Nyamagana, wapinzani
walipewa haki ya kura kuhesabiwa
upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua
kwenda mahakamani kupinga matokeo
ya uchaguzi katika majimbo haya.
Tunataka sote tujiridhishe kwamba
utashi wa wananchi umeheshimiwa.
Bado tunaendelea kukusanya taarifa
za maeneo mengine kama kulikuwa na
ukiukwaji mkubwa uliobadilisha
matakwa ya wapiga kura. Hata hivyo,
tunakiri kwamba kwenye maeneo
mengi tulikopoteza viti vya Ubunge,
tumepoteza kihalali, hatuna
malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya
wananchi, na tutafanya tathmini baada
ya uchaguzi ili tubaini makosa na
kuyarekebisha.
MAONI YA WAANGALIZI WA
UCHAGUZI
CCM imepokea maoni ya awali ya
waangalizi wa uchaguzi. Tumefarijika
kwamba karibu wote wametoa kauli ya
pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa
wa haki na huru, uliofanyika kwa
uwazi na kwa amani – na kwamba
changamoto zilizojitokeza ni ndogo na
zimetokea katika maeneo machache
kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo
ya uchaguzi yanayotangazwa sasa.
Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa
kwa wadau mbalimbali kuhusu namna
ya kuboresha mchakato wa uchaguzi
kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha
demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli
za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi
uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo
yanayotangazwa sasa ni kielelezo
sahihi cha utashi wa Watanzania
kuhusu viongozi wanaowataka.
MALALAMIKO YA UKAWA
Tumesikia malalamiko ya viongozi wa
UKAWA kupitia mkutano wao na
waandishi wa habari jana.
Tumeshangazwa na kauli kwamba
hawakubali matokeo ya Urais
yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo,
matokeo ya Ubunge wanayakubali na,
kule wanakoshinda,
wanayasheherekea. Tunashangazwa
kwasababu
Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni
hiyo hiyo iliyoandaa uchaguzi wa
Wabunge, wasimamizi ni walewale,
vituo ni vilevile, na sheria na taratibu
zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya
matokeo walizosaini wakala wao
kwenye vituo vya kupiga kura,
zimegawanywa katika sehemu
(columns) tatu: Urais, Ubunge na
Udiwani. Mawakala wao walisaini
fomu hizo kwenye vituo vya kupiga
kura. Wameanza kuwa na matatizo na
matokeo haya baada ya kuona
mwelekeo wa kushindwa. Kama
mwelekeo ungekuwa tofauti,
wangekuwa na imani na Tume,
wasimamizi na taratibu zote.
Tunaomba ifike pahala sasa kwamba,
katika kuijenga demokrasia yetu na
kuliimarisha taifa letu, tuanze
utamaduni mpya wa anayeshindwa
kunyanyua simu kumpigia
anayeshinda na kumpongeza. Nafasi
ya mwisho aliyonayo Mgombea wa
UKAWA kuendelea kujijengea heshima
katika jamii yetu, na kuwa
mwanademokrasia, ni kwa kufanya
hivyo siku Dkt. Magufuli
atakapotangazwa mshindi.
Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea
bora na kuwanadi na kutengeneza sera
bora na kuzinadi, pamoja na rekodi
yetu katika uongozi wa nchi, ndio njia
zetu pekee za ushawishi. Katika
uchaguzi huu, wananchi wamefanya
maamuzi yao kwa uhuru na utashi,
ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita
ambao tuliwasimamisha kama
wagombea wetu katika majimbo
mbalimbali. Nguvu na utashi wa
wananchi umejidhihirisha katika
uchaguzi huu.
Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia
kufikia ukingoni, tutawapata
madiwani, wabunge na Rais,
tunapaswa kuendelea na maisha na
tuwape nafasi watutumikie. Jitihada
tunazoziona sasa za viongozi wa
UKAWA za kuendeleza siasa za
uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu
kwa njia za vurugu na maandamano
hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani
kitendo cha wafuasi wa UKAWA
kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya
Mbozi.
Amani ya nchi hii ina thamani kuliko
hitaji la madaraka la mtu yoyote.
Wenzetu wa UKAWA wana haki ya
kulalamika lakini hawana haki ya
kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa
kuwakusanya vijana na kuwaingiza
mitaani wafanye vurugu na
kuhatarisha maisha, kuharibu mali na
kusimamisha shughuli za watu
wengine.
Tunawaomba Watanzania waendelee
na shughuli zao kama kawaida huku
kila mmoja akitambua wajibu wake wa
kuilinda amani ya nchi yetu.
January Makamba
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya
CCM
28.10.2015 






Post a Comment

Previous Post Next Post