RAIS Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji pamoja na
viongozi wa kitaifa, katika kumuaga Mwenyekiti wa Chama cha DP,
Mchungaji Christopher Mtikila aliyekufa kwa ajali hivi karibuni mkoani
Pwani.
Katika shughuli hiyo, viongozi wengi waliohudhuria walimuelezea
Mtikila kuwa ni mwanaharakati wa mageuzi, aliyeipigania Tanganyika mpaka
kifo chake, lakini pia alisimamia na kuheshimu taratibu za kisheria na
kutaka mabadiliko bila uoga.
Rais Kikwete alifika katika shughuli hiyo ya kumuaga Mtikila
iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, akiambatana na Makamu wa Rais,
Dk Mohammed Gharib Bilal na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi.
Viongozi wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni Makamu wa Kwanza wa
Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF), Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi, Msajili wa zamani wa vyama hivyo, John Tendwa na Makamu
Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.
Pia walikuwepo Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Mziray
ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha PPT-Maendeleo, Makamu Mwenyekiti wa
Chadema, Profesa Abdallah Safari na Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Dotnata
Rwechungura.
Akizungumza katika shughuli hiyo ya kumuaga Mtikila ambaye jeneza
lake lilifunikwa kwa bendera ya Tanganyika, Msajili wa Vyama vya Siasa,
Mutungi aliwataka watanzania kumuenzi mchungaji huyo kwa matendo yake ya
kuchukia vurugu na badala yake aliamini zaidi katika sheria.
“Mchungaji Mtikila atakumbukwa kwa misimamo yake mikali. Alipenda
kusimamia kile anachokiamini. Lakini kubwa zaidi alitoa mchango katika
nyanja ya Sheria, kwa sasa huwezi kuzungumzia masuala ya sheria hususani
haki za binadamu bila kumtaja Mtikila,” alisema Mutungi.
Alisema kupitia sekta ya Sheria, mwanaharakati huyo alifanikisha
mabadiliko kadhaa, ikiwemo kuingizwa kwenye Katiba kwa kifungu
kinachoruhusu mgombea binafsi, lakini pia alifanikisha kubadilishwa kwa
kifungu kinachohusu maandamano.
“Huyu alikuwa ni mpambanaji, alifungua kesi nyingi kwa kuwa aliamini
katika kufuata sheria na si kuandamana au kufanya vurugu. Naomba
tumuenzi kwa kutopenda kushinikiza fujo na maandamano, vyombo vya sheria
vipo kama kuna tatizo tuvitumie kutafuta haki,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Dk Bilal alimtaja Mchungaji Mtikila kuwa alikuwa ni
mtu jasiri, aliyeshirikiana na wenzake bila kujali tofauti za mitazamo
waliyonayo. “Mimi nilimfahamu Mtikila kupitia uanaharakati wake wa
kutaka mabadiliko, ni kweli alikuwa anataka sana kuirejesha Tanganyika,
lakini pamoja na tofauti za fikra zetu, alikuwa anakuja hadi ofisini
kwangu kipindi kile nilikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Sayansi, Mawasiliano
na Teknolojia na tulikuwa tunazungumza sana,” alisema.
Aliwataka watanzania kuiga mfano wa matendo ya Mtikila, kwani kwa
sasa nchi inataka watu kama hao wenye mawazo mapya na hawaogopi kuyatoa
na kuyatetea bila kudharau mawazo na fikra za wengine.
Maalim Seif, kwa upande wake, alisema alifahamiana na Mtikila kupitia
harakati zake za kisiasa na kubainisha kuwa ni mtu anayejiamini, asiye
uoga na mwenye kuajimini na kusimamia kile anachokiamini.
Mziray alisema anaipongeza Serikali kwa kitendo chake cha
kushirikiana na familia ya Mtikila kwa hali na mali, bila kujadili kuwa
ni mwanaharakati wa mabadiliko, jambo alilosisitiza kuwa hiyo ndio
Tanzania inayotakiwa kwa sasa.
Makamu Mwenyekiti wa DP, Peter Mwagila alibainisha kuwa chama hicho
kimepata pigo na pengo kubwa kwa kuondokewa na mwenyekiti wao, ambaye
pia pamoja na kuwa muasisi wa chama hicho, ni mwanaharakati wa mageuzi
aliyepigania nchi yake ya Tanganyika.
“Mtikila ndoto zake zilikuwa ni kurejeshwa kwa Tanganyika ambayo
iliondolewa kwenye ramani ya dunia tangu mwaka 1962, alitaka kuwepo na
Rais wa Tanganyika, Katiba, wabunge na mamlaka zote za nchi ya
Tanganyika. Lakini pia alipinga rushwa, ufisaidi na kuwachukia viongozi
wanaojilimbikizia mali,” alisema.
Alisema chama hicho kitahakikisha kinaendeleza na kusimamia harakati
zote zilizoanzishwa na Mtikila ikiwemo kuidai Tanganyika. Msemaji wa
familia ya mchungaji huyo, Peter Mayani, wakati akisoma wasifu wa
Mtikila, alisema mwanaharakati huyo alibobea katika fani za sheria,
uchumi na masoko na aliwahi kuajiriwa Mahakama Kuu na Shirika la Ndege
la Afrika Mashariki, ambalo alilitumia kutoroshea wanaharakati wa chama
cha Frelimo.
Alisema Mtikila aliokoka rasmi mwaka 1983 na kuanzisha Kanisa la
Pentekoste la Full Salvation na mwaka 1990 alianza harakati za ukombozi,
zilizoshinikiza kuanzishwa kwa vyama vingi mwaka 1992. Pia alianzisha
chama cha DP, ambacho kilichelewa kupata usajili wake hadi mwaka 2000.
Mtikila baada ya kuagwa alisafirishwa kwenda kijijini kwao Milo,
wilayani Ludewa mkoani Njombe ambako anatarajiwa kuzikwa leo. Marehemu
ameacha mjane Georgia Mtikila. Askofu wa Kanisa la Ufunuo, Nabii Paul
Bendera, aliwataka watanzania kutambua kuwa wote ni wageni duniani na
kwamba kila mtu bila kujali ni nani duniani na ana cheo gani iko siku
yake atakufa.
“Kwa sasa hali imekuwa ngumu na mbaya nawaomba ndugu zangu tuwe
makini, lakini kubwa zaidi kila mtu amheshimu maisha ya mwenzake tuweke
upendo na amani mbele na hii iwe ndio kipaumbele chetu. Naomba Serikali
nayo iongeze juhudi za kuwalinda wananchi wake,” alisisitiza.
Mchungaji Daudi Mwaijojele, alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania
kuacha uchafu na kumrejea Mungu, ili kutengeneza maisha yao ya baadaye
pindi watakapokufa. “Nawaomba acheni uchangudua, ufisadi na michepuko
tena hiyo michepuko ndio inaleta magonjwa kama vile Ukimwi majumbwani na
kusambaratisha familia,” alisema.
Mtikila alikufa kwa ajali ya gari aina ya Toyota Corolla, lenye namba
za usajili T 189 AGM maeneo ya Msolwa wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Alikuwa akitokea Njombe kwenda Dar es Salaam.